SHAURI linalowakabili washtakiwa tisa wanaotuhumiwa kumuua mtoto aliyekuwa na ualbino Asimwe Novath mkoani Kagera, leo wawamefikishwa tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba.
Kesi hiyo ambayo imeanza kurindima hivi karibuni inaonekana kuwavutia baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Bukoba na pembezoni mwa mji huo na kufanya mahakama kufurika kutokana na wingi wa wasikilizaji katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba.

Washtakiwa hao tisa ambao ni Padre Elpidius Rwegoshora na Baba wa Marehemu Novart Venant huku wengine waliofikishwa mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba, ElipokeaYona Wilson ni Nurdin Ahamada, Ramadhan Celestine, Rwenyagira Bulchad, Dunstan Buchard, Faswiu Athuman, Gozberth Alkardna na Dezdery Evargist.
Soma: Paroko, baba mbaroni mauaji ya Asimwe
Wakili wa Serikali Erick Mabagala amesema upande wa Jamhuri unaendelea na hatua za kusajili shauri hilo katika Mahakama Kuu na kuomba shauri hilo liahirishwe tena kwa ajili ya kutajwa tena kwani mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria ya kulisikiliza.
Padre Elpidius Rwegoshora amemtambulisha Mathias Rweyemamu kuwa Wakili wake katika shauri hilo.
Washtakiwa hao tisa wamerejeshwa tena rumande hadi shauri hilo litakapotajwa tena Julai 26 2024.
Taarifa ya Msemaji wa jeshi la Polisi DCP David Misime Juni mwaka huu ilisema washukiwa hao walikamatwa na viungo vya mwili vinavyo sadikiwa kuwa ni vya marehemu aliyekutwa ameuawa na mwili wake kutelekezwa kwenye karavati Juni 17.
“Polisi kwa kushirikiana na raia wema wanaochukia vitendo vya kinyama kama hivyo walianza msako mkali kuanzia Mei 31, 2024 hadi usiku wa kuamkia Juni 19, 2024 ambapo watuhumiwa tisa wamekamatwa,” alisema DCP Misime.