Kesi ya rufaa ya Sabaya kusikilizwa Januari 17

KESI ya rufaa iliyofunguliwa na upande wa Jamhuri kupinga kuachiwa huru aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai ole Sabaya (35) na wenzake watano sasa inatarajiwa kusikilizwa Januari 17 mwaka huu.

Kesi hiyo ilitajwa jana mbele ya Hakimu Mfawidhi Mkoa wa Arusha, Fadhili Mberwa na Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Akisa Mhando alimwomba hakimu huyo kuahirisha kesi hiyo ili Ofisi ya Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Arusha itekeleze wajibu wa kisheria wa wito wa tangazo magazetini kwa mara ya tatu kwa mujibu wa sheria ili wajibu rufaa wengine waweze kuja mahakamani.

Sabaya jana alikuwepo mahakamani na mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo, Enock Mnkeni lakini wajibu rufaa wengine waliokosa kufika jana ni pamoja na John Aweyo, Slvester Nyegu, Jackson Macha pamoja na Nathan Msuya.

Hata hivyo, Wakili Fridorini Bwemelo anayemtetea Aweyo alimweleza hakimu kuwa anaomba rufaa hiyo iendelee bila mteja wake kuwepo mahakamani kwani kisheria inaruhusiwa.

Baada ya hivyo hakimu alihirisha hadi Januari 17 mwaka huu na kusema kuwa kesi hiyo siku hiyo itakuja kwa ajili ya kusikilizwa baada ya matakwa ya kisheria ya matangazo kukamilika.

Awali Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Judith Kamala ambaye shauri hilo mara ya mwisho lilisikilizwa kwake alisema hati ya wito ilishatangazwa katika magazeti mawili ya Desemba 17 na Desemba 20 mwaka huu, lakini sheria inasema matangazo hayo ya wito yanapaswa kutangazwa mara tatu katika magazeti.

Katika rufaa hiyo, Sabaya anatetewa na mawakili wawili Mosses Mahuna na Faudhia Mustapher na wajibu rufaa wengine wanatetewa mawakili Silvester Kahunduka na Fridolini Bwemelo. Rufaa hiyo inasikilizwa na Jaji Salma Maghimbi aliyekuja rasmi kusikiliza rufaa hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.

Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, Sabaya na wenzake waliachiwa huru na Hakimu Patricia Kisinda katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi kwa kile kilichoelezwa kuwa hakukuwa na ushahidi wowote wa kuwatia hatiani watuhumiwa.

Hakimu Kisinda mbali ya hilo pia alisema kuwa watuhumiwa hao sita hawakupewa nafasi ya kuulizwa maswali ya dodoso kutoka kwa mawakili wao hivyo walinyimwa haki kwa mujibu wa sheria.

Kutoka na hali hiyo Jamhuri ilikata rufaa kupinga hukumu hiyo kwa kutoa sababu lukuki ikiwemo kuwa hakimu Kisinda alikosea kisheria katika hukumu yake kwani ushahidi ulitolewa katika mahakama hiyo ulitosha kuwatia hatiani watuhumiwa na watuhumiwa walipewa nafasi kisheria kuulizwa maswali na mawakili wao kama miongozo ya kisheria inavyoelekeza.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x