MKAZI wa Kijiji cha Donge Wilaya ya Kaskazini Unguja, Mcha Khamis Kombo (25) amefikishwa katika Mahakama ya Vunga, Unguja akishtakiwa kwa kukutwa na kete 594 za dawa za kulevya aina ya heroin.
Mwendesha mashtaka, Ali Yussuf alisema mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Salma Hassan Ali kwamba mshtakiwa alikamatwa na dawa za kulevya Oktoba 5, mwaka huu huko Donge baada ya kutiliwa shaka na wananchi ambao waliamua kumkamata na kumfikisha katika vyombo vya sheria.
Hata hivyo, mshtakiwa alikataa mashtaka na hivyo Jaji Salma aliahirisha kesi hiyo na kuipanga kwa hatua nyingine Novemba 14 mwaka huu ambapo mashahidi wanatarajiwa kuanza kutoa ushahidi wao dhidi ya mshitakiwa.
Mahakama ya Vuga ilikataa kumpatia dhamana mshitakiwa kwa maelezo ya kiasi cha dawa za kulevya kuwa kikubwa.