Khoja Shia Ithnasheri waandaa upimaji afya bure

DAR ES SALAAM; Jumuiya ya Khoja Shia Ithnasheri Mkoa wa Dar es Salaam, imeandaa kambi ya bure ya afya na macho kwa siku tatu kuanzia Ijumaa hadi Jumapili ya wiki hii viwanja vya Mnazi Mmoja yaliyopewa jina la Mafunzo ya Imam Hussain (A.S) ambaye alifariki huko Karbala nchini Iraq miaka 1400 iliyopita.
Kambi hiyo ya bure ni mwendelezo wa jitihada za jumuiya hiyo katika utoaji huduma kwa jamii bila malipo na huduma hiyo itaanza saa mbili asubuhi hadi saa 11 jioni.
Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaji Mohamedraza Dewji, amesema kuwa kambi hiyo ambayo mwaka jana ilihudumia maelfu ya wananchi, inaleta pamoja wataalamu wa afya, taasisi mbalimbali, na mashirika ya tiba kutoka ndani ya Tanzania, katika juhudi ya pamoja ya kuwafikia wale wasio na uwezo wa kupata huduma hizi kwa urahisi.
Amesema kuwa mbali na utolewaji wa huduma hizo katika kambi hiyo ya siku tatu pia kutatolewa miwani na dawa bure, pamoja na uchunguzi wa mtoto wa jicho (cataract.)
Aidha, Mwenyekiti huyo amesema kuwa kutatolewa bure vipimo vya sukari, shinikizo la damu, uzito na urefu (BMI) na elimu juu ya ugonjwa wa afya ya akili, uchunguzi wa saratani ya matiti na shingo ya kizazi kwa kina mama kwa ushirikiano na taasisi ya kansa ya Ocean Road.
Vile vile, Mohamedraza amesema kuwa kutakuwa na uchangiaji wa damu kwa kushirikiana na Taasisi ya Damu Salama, huduma hizo zitatolewa bila gharama yoyote, na zinalenga kuwahudumia wananchi wote.
Amesema jina la kambi hiyo linatokana na Imam Hussain (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), ambaye alisimama kwa misingi ya haki, huruma na huduma kwa binadamu katika tukio mashuhuri la Karbala.
“Waanzilishi wa kambi hiyo wanasema kuwa lengo ni kugeuza mafunzo ya Karbala kuwa vitendo vya huruma vinavyogusa maisha ya watu, hasa walioko pembezoni ,” amesema Mwenyekiti huyo.
Amesema kambi hii imekuwa si tu chanzo cha afya bora kwa wananchi, bali pia ni darasa la maadili, likiunganisha watu wa makundi mbalimbali kwa msingi wa utu na huduma.
Ushiriki wa Jamii ya Waislamu wa Shia katika kambi hiyo inayoandaliwa kila mwaka na jamii ya Waislamu wa Shia wa Mkoa wa Dar es salaam maarufu kama Khoja Shia Ithna-Asheri Jamaat , hujielekeza katika matendo ya kusaidia waliodhulumiwa, wagonjwa, na wahitaji, wakisisitiza kuwa dini ya kweli hujidhihirisha katika matendo mema.