Kibano wamiliki wa nyumba, hoteli

SERIKALI imewataka wenye nyumba na wamiliki wa hoteli kufuatilia wapangaji wao mara kwa mara ili kujiridhisha kuwa wanaoishi katika nyumba hizo ni wapangaji halali waliosaini mkataba wa upangaji na wenye nyumba au kwenye hoteli.
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba alisema hayo alipotembelea na kukagua ujenzi wa soko na stendi mpya Bunju wilayani Kinondoni mkoani Dar es Salaam.
Dk Mwigulu amesema ipo tabia imeibuka ya wapangaji kuwa madalali kwa kupanga nyumba ya mtu kisha na wao kuipangisha kwa kundi la watu kwa kigezo cha kusaidia wananchi wenye uhitaji na kipato cha chini huku gharama ya nyumba ikipungua.

Alisema wema wa namna hiyo siyo wema kwa sababu unakuja kuliponza taifa kwani baadhi ya watu wanaopangishwa katika nyumba hizo hawana nia nzuri kwa maendeleo ya nchi.
Ili kukabiliana na hali hiyo, amezitaka mamlaka za serikali za mitaa na wamiliki wa nyumba na hoteli kupitia upya utaratibu wa upangishaji kwa lengo la kumjua mpangaji, lengo lake, idadi ya wapangaji wanaoingia katika nyumba na uraia wao.
SOMA: Dk. Mwigulu akagua hali ya maji Ruvu Chini
Dk Mwigulu alieleza kuwa sababu za kuchukua hatua hizo ni kutokana na kasi iliyopo kwa sasa ya kulundikana
kwa wapangaji katika nyumba moja kuwa kubwa.
“Leo hii tumeona madhara ya usalama kwa hawa wageni wanaokuja na sisi Watanzania kwa wema wetu tunachukulia kawaida… Tunaenda kwenye nyumba tunapangisha Dola (za Marekani) 5,000 halafu tuliyempangisha anapangisha watu wengine 60 na kupokea Dola 30,000,” alieleza Waziri Mkuu.
Aliongeza: “Analundika watu wageni haijulikani wanachokifanya, mwenye nyumba hajui nyumba yake inaingiza fedha kiasi gani”.

Alisema kila mpangaji ahakikishe ana taarifa za wapangaji wake na kwamba ndani ya nyumba yake wanaishi watu wangapi ili iwe rahisi kugundua njama zozote zinazoweza kupangwa kupitia nyumba yake.
Alisema wakati watu hao walitakiwa kufikia katika nyumba za wageni ambako ingekuwa rahisi kupata taarifa zao, Watanzania wanawapokea watu hao katika nyumba zao bila kufahamu kinachopangwa na watu hao katika nchi yao.
Kadhalika, Dk Mwigulu ameiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi pamoja na Jeshi la Polisi kuacha mara moja kushikilia pikipiki na bajaji ambazo zinatakiwa kulipa faini kutokana na makosa ya barabarani.
Alisema badala ya kushikilia chombo hicho, mwenye chombo kwa kuwa ndio ofisi yake arudishiwe akafanye kazi apate fedha za kulipa faini.
Alielekeza bajaji na pikipiki zinazotakiwa kushikiliwa kuwa ni zile zilizokutwa zikisafirisha dawa za kulevya au silaha kwa maana ya kushikiliwa kwa makosa ya jinai.
Katika hatua nyingine, amedokeza kuwa utekelezaji wa ahadi za Rais Samia Suluhu Hassan kwa Watanzania ndani ya siku 100 zinaendelea kutekelezwa kwa kasi.
Alisema katika sekta za elimu na afya, ajira za watumishi zitatangazwa Januari 10, 2026 baada ya siku 10 za usaili zilizoanza Desemba 10, 2025 ambapo katika sekta ya afya watumishi 5,000 wataajiriwa na sekta ya elimu wataajiriwa walimu 7,000.
Aliongeza kuwa mwezi huo huo wa Januari, Bima ya Afya kwa wote itaanza kutekelezwa huku akitoa agizo wananchi wote wanaotaka kuchukua maiti za ndugu zao kutozuiwa kwa kigezo cha malipo ya matibabu kabla mgonjwa hajafariki dunia.



