Kibu arejea kuikabili Namungo

DAR ES SALAAM; MSHAMBULIAJI Kibu Dennis amerejea kwenye kikosi cha Simba baada ya kukosa michezo miwili iliyopita ya timu hiyo kutokana na majeraha.

Kibu aliyeumia kwenye ushindi wa timu hiyo wa mabao 3-0 dhidi ya Tabora United, Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora, alikosa mechi dhidi ya Fountain Gate na Tanzania Prisons ambazo Simba ilitoka sare ya bao 1-1 na kushinda mabao 5-0.

Akizungumza na HabariLEO jana, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alithibitisha kurejea kundini kwa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Tanzania.

“Taarifa njema ni kwamba Kibu amepona majeraha yake aliyopata kwenye mchezo dhidi ya Tabora United na anafanya mazoezi na wenzake, kama itampendeza kocha Fadlu anaweza kumtumia kwenye mechi ijayo dhidi ya Namungo,” alisema Ahmed.

Ahmed alisisitiza malengo ya timu hiyo kushinda mchezo huo wa Februari 19, na mengine yote kwenye ligi hiyo ili kutimiza azma yao ya kushinda ubingwa huo msimu huu.

Simba inashika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ikiwa na pointi 47 huku Yanga wakiongoza wakiwa na pointi 49 lakini watoto hao wa Jangwani wana mchezo mmoja zaidi ya mpinzani wao.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button