SHEKHE wa Mkoa wa Kigoma, Hassan Kiburwa amewaongoza waumini wa kiislam mkoani humo kusoma dua maalum ya kumuombea afya njema Rais Samia Suluhu Hassan.
Shekhe kiburwa ameongoza dua hiyo iliyofanyika katika Msikiti wa Muumini Ujiji mjini Kigoma ikihudhuriwa na mashekhe wa wilaya zote za Kigoma walio chini ya Baraza Kuu la Waislam (BAKWATA) na Jumuiya mbalimbali za waislam mkoani humo.
Akizungumza katika dua hiyo, shekhe huyo amesema kazi kubwa iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kusimamia miradi ya maendeleo ambayo inalenga maisha ya Watanzania ndiyo iliyowasukuma waislamu kusoma dua hiyo.
Kwa upande wake Kadhi wa Mkoa Kigoma, Idrisa Kitumba alimweleza Rais Samia kama kiongozi ambaye anatokana na vitabu vya dini hasa majina yake ya kwanza Samia na mwisho Hassan ambayo yanatafsiri kubwa hivyo kufanya mambo makubwa kwa ajili ya Watanzania inasadifu kulingana na jina lake.
Shekhe Mkuu wa Taasisi ya Iswati Istiqma, Dabas Khalfan Kiumbe amesema kuwa vikao vya CCM vilivyopitisha jina la Rais Samia kugombea tena uraisi wa Tanzania kupitia chama hicho kwa mwaka huu wa uchaguzi havikukosea.
Awali Katibu Mwenezi wa CCM Kigoma, Deogratius Nsokolo ambaye alikaribishwa kutoa salam za Chama alisema kuwa Rais Samia anastahili kuombea dua hiyo ili afya yake isitetereke.
Mkuu wa Wilaya Kigoma, Rashid Chuachua akimwakilisha Mkuu wa Mkoa Kigoma amesema kuwa kwa niaba ya serikali wanatoa shukrani kubwa kwa kuona na kuthamini mchango wa Rais Samia katika kuwaletea maendeleo Watanzania hivyo wanapokea dua hiyo wakizidi kumuomba Mungu iweze kufanya kazi na kuwa kinga kwake azidi kuwatumikia Watanzania.