Kihenzile aipa tano serikali kufufua uwanja wa ndege Iringa

IRINGA: NAIBU Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile ameishukuru serikali kwa kuutendea haki Mkoa wa Iringa kwa kujenga uwanja wa ndege mkoani humo ambapo zaidi ya Sh bilioni 60 zimetumika kufufua uwanja huo wa kihistoria mkoani Iringa.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba uliofanyika katika Viwanja vya Stendi ya Luganda mkoani Iringa, Kihenzile amesema kukamilika kwa upanuzi wa ujenzi wa kiwanja cha Ndege cha Nduli -Iringa kumesaidia kukuza shughuli za kibishara, kilimo na utalii.
Aidha Naibu Waziri ameeleza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk Samia Suluhu kufufua upya reli ya Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) ambapo amesema kukamilika kwa mradi huo kutarahisisha usafirishaji wa mazao yanayozalishwa wilayani Kilolo kupitia treni hiyo.
Katika hatua nyingine Kihenzile ameeleza dhamira ya Serikali kurejesha hadhi ya reli ya TAZARA mkoani Iringa na maeneo mengine ndio maana mwaka 2022 Rais Dk Samia Suluhu Hassan alisaini mkataba wa ukarabati kwa thamani ya Sh trilioni 3.3 jambo litakalo rahisisha shughuli mbalimbali za kiuchumi.
“Hii ni reli ya kihistoria, ni kielelezo cha uhuru wetu tulipoamua kuanza kujitawala ni alama ya ya watawala wetu viongozi wa wazelendo wa nchi hii walipoamua kuunganisha nchi zetu, ilijengwa ikiwa na uwezo wa kubeba mzigo wa tani milioni tano lakini miaka yote ya kuanzishwa kwake haikuwa na uwezo wa kubeba mizigo hiyo kwasababu mbalimbali ikiwemo uharibifu wa miundombinu na ikasababisha wanairinga kujikuta hawanufaiki na reli hii” lakini Dk Samia Suluhu Hassan kuamua kusaini mkataba wa ukarabati wa reli hiyo kutarejesha hadhi ya reli hiyo.” amesema Kihenzile.
Pia Kihenzile amepongeza mapinduzi yaliyofanyika katika sekta ya bandari ikiwemo maboresho Pamoja na kuleta watu wa kuendesha bandari hizo ambapo matunda yake yameonekana.



