Kihenzile: Kura kwa Dk Samia na CCM ni maendeleo, matumaini mapya

Na Frank Leonard, Mufindi

Mgombea Ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Mufindi Kusini, David Kihenzile, ameongoza mamia ya wananchi wa jimbo hilo katika mkutano wa kufunga kampeni uliojaa hamasa na matumaini, akiwataka Watanzania wote kujipanga kwa amani, umoja na maendeleo kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.

Akiomba kura za CCM na wagombea wake katika mkutano uliofanyika katika kata ya Malangali, Kihenzile alisema uchaguzi huu ni fursa ya kuthibitisha imani kwa serikali ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan, ambaye amerejesha matumaini mapya kupitia kasi ya maendeleo, uwajibikaji na utulivu wa nchi.

“Tanzania ipo kwenye njia sahihi ya maendeleo. Kura zetu za Oktoba 29 zitaamua mustakabali wa taifa letu — kura kwa Dkt. Samia, kura kwa Kihenzile, ni kura ya amani, utulivu na kazi iendelee,” alisema Kihenzile huku akishangiliwa.

Ameeleza kuwa katika kipindi chake cha uongozi, miradi ya barabara, nishati, afya na elimu imepiga hatua kubwa, akibainisha kuwa zaidi ya asilimia 75 ya vitongoji vya jimbo hilo sasa vimeunganishwa na umeme, huku barabara za kiuchumi zikijengwa.

“Tulipoanza mwaka 2020, vitongoji vyenye umeme vilikuwa chini ya 100 kati ya 325, leo tupo zaidi ya asilimia 75 — ni hatua kubwa. Lengo letu ni kumaliza vilivyosalia ili kila kaya ifikie mwanga wa maendeleo,” alisema.

Katika sekta ya afya, Kihenzile alisema ujenzi wa vituo vya afya vipya, huduma za maji safi, na uwezeshaji wa vijana kupitia ruzuku ya mbolea na mikopo midogo ni kielelezo cha dhamira ya serikali ya CCM katika kuinua maisha ya wananchi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yassin, aliwahimiza wananchi kuendelea kuwa na imani na mchakato wa uchaguzi, akisisitiza kuwa unafanyika kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na si kwa matakwa ya chama chochote.

“Uchaguzi huu ni wa kikatiba, wa amani na wa haki. Rais wetu, Amiri Jeshi Mkuu Dk Samia Suluhu Hassan, ameelekeza hakuna vurugu, hakuna hofu. Kila Mtanzania ajitokeze kupiga kura kwa utulivu na kurejea nyumbani kwa amani,” alisema Yassin.

Amesisitiza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kuhakikisha kila mwananchi anatekeleza haki yake ya kikatiba bila bughudha, huku akiomba kura za kutosha kwa Dk Samia, Kihenzile, na madiwani wote wa CCM.

Naye Mbunge Mteule wa Baraza la Vijana la CCM (UVCCM), Jasmini Ng’umbi, aliwataka wananchi wa Mufindi Kusini kujitokeza mapema Oktoba 29 na kumpa heshima Rais Dk Samia kwa kura za ushindi.

“Mmeona kazi iliyofanyika. Huu si wakati wa kurudi nyuma, ni wakati wa kuthibitisha imani yetu. Twende tukamchague Dk Samia, tumchague Kihenzile, na madiwani wote wa CCM,” alisema kwa hamasa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button