Kiingereza kuwa kigezo wanufaika Samia Scholarship

ARUSHA: WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema wanafunzi wanaolenga kujiunga na Chuo Kikuu cha Johannesburg nchini Afrika Kusini kupitia programu ya Samia Scholarship wanapaswa kupata daraja A katika somo la Kiingereza katika mtihani wa Kidato cha Nne ili kukidhi vigezo vya udahili.
Amesema pamoja na wanafunzi kuwa na ufaulu wa juu katika masomo ya sayansi, ikiwamo Fizikia, Kemia na Hisabati, uwezo wa lugha ya Kiingereza ni muhimu kwa kuwa vyuo vikuu vya kimataifa vina masharti maalumu ya lugha kabla ya kuwaruhusu wanafunzi kujiunga na masomo.
Profesa Mkenda amesema hayo wakati akizungumza na wanufaika wa programu hiyo wanaojiandaa kujiunga na vyuo mbalimbali vya nje ya nchi, ambao kwa sasa wanaendelea na maandalizi katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), mkoani Arusha.
Amesema serikali inaendelea kuwaandaa wanafunzi kwa ajili ya kujiunga na vyuo vikuu mbalimbali vya kimataifa, vikiwamo Chuo Kikuu cha Johannesburg na vyuo vilivyopo nchini Ireland, huku akiwataka kuzingatia masharti ya udahili na taratibu za ufadhili.
Akizungumzia maandalizi hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Samia Scholarship, Profesa Emeritus Mgaya, amesema Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeingia makubaliano na Chuo Kikuu cha Johannesburg kwa ajili ya kuwasomesha vijana wa Kitanzania katika taaluma za Sayansi ya Data, Akili Unde na fani zinazohusiana nazo.
Amesema wanafunzi wanaojiandaa kwenda kusoma katika vyuo vya nje ya nchi wanapaswa kufanya mitihani ya kimataifa ya Kiingereza na kupata alama zinazokidhi viwango vinavyotakiwa na vyuo husika.
Kutokana na hali hiyo, Profesa Mgaya amewataka walimu wa shule za msingi na sekondari kuimarisha ufundishaji wa lugha ya Kiingereza ili kuwajengea wanafunzi msingi imara utakaowawezesha kutumia fursa za elimu ya juu katika vyuo vya kimataifa.



