MWANAMKE mkazi wa Kitongoji cha Chang’ombe katika Kijiji cha Kaloleni wilayani Songwe, ameuawa na mwili kukatwa vipande vipande huku ikidaiwa kuwa muuaji ana tatizo la afya ya akili.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Alex Mukama amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kumtaja mwanamke aliyeuawa kuwa ni Bertha Shugha (69) na akasema mtuhumiwa wa mauaji hayo anashikiliwa na polisi.
Kamanda Mukama alimtaja mtu aliyefanya mauaji hayo kuwa ni Lazaro Adamson (40), mkazi wa Kaloleni ambaye anadaiwa kufanya mauaji hayo usiku wa kuamkia Novemba 13 mwaka huu katika Kitongoji cha Chang’ombe kilichopo Kijiji cha Kaloleni wilayani Songwe.
Wakizungumzia tukio hilo, baadhi ya wakazi wa Kitongoji cha Chang’ombe walisema walishtukia uwepo wa mauaji hayo baada ya kuona damu nyingi zikiwa zimezagaa kwenye nyumba ya mtuhumiwa, jambo ambalo halikuwa la kawaida.
“Tulipoona damu ile, tulimuuliza Lazaro, akatueleza kuwa alikuwa amechinja mbuzi,” alisema Jesca, mmoja wa wakazi wa kijiji hicho.
Alisema majibu hayo yaliwashangaza kwa kuwa hawakuwahi kumuona mtuhumiwa akifuga mbuzi na zaidi walijua kuwa alikuwa na matatizo ya akili, hivyo waliamua kutoa taarifa polisi ili kujua mbuzi aliyechinjwa alikuwa wa nani.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Songwe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo, Simon Simalenga amekiri kuwepo kwa tukio hilo na kudai kuwa hilo ni tukio lenye kushangaza zaidi kulishuhudia tangu ashike wadhifa wa Ukuu wa Wilaya.
Alisema kuwa baada ya kukamatwa kwa mtuhumiwa yeye mwenyewe alilazimika kufika kituo cha polisi kumuona na kufanya mahojiano naye.
Simalenga alisema kabla ya kufanya mahojiano naye alikwenda kuuona mwili wa marehemu, lakini alishuhudia ukiwa umekatwa vipande vipande na baadhi ya viungo vikiwa hivionekani.
Simalenga alisema aliushuhudia mwili wa marehemu ukiwa umekatwa kichwa, kiwiliwili kikiwa kimetenganishwa kuanzia kiunoni, mikono ikiwa kivyake na nyayo za miguu pia zikiwa kivyake.
Kwa mujibu wa Simalenga, mtuhumiwa alikiri kumuua mtu huyo kwa kumpiga panga kisogoni na katikati ya kichwa na kwamba alipopoteza maisha ndipo akaanza kumkatakata.
Aliongeza kuwa jitihada za polisi kutafuta baadhi ya viungo vya mwili wa marehemu ambavyo vilikuwa havionekani zilifanyika ambapo baada ya jitihada hizo walifanikiwa kuvipata vikiwa vimefichwa katika shimo la choo ambalo lilikuwa halitumiki.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa viungo vya marehemu vilivyopatikana vimehifadhiwa katika Hospitali ya Mwambani iliyopo Mkwajuni wilayani humo.