TIMU ya taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ itafungua pazia la michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa kuikabili Burundi Januari 3, Uwanja wa Gombani, Pemba.
Ratiba iliyotolewa na Kamati ya Kombe la Mapinduzi hivi karibuni inaonesha ndugu zao Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ itaikabili Burkina Faso siku inayofuata.
Januari 5 kwenye uwanja huo, timu ya taifa ya Kenya maarufu ‘Harambee Stars’ itaikabili Burundi huku Burkina Faso ikikutana na Uganda ‘The Cranes’ Januari 6.
Zanzibar Heroes itarudi tena uwanjani kucheza na Harambee Stars Januari 7 wakati Kilimanjaro Stars itacheza na Uganda Januari 8.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Cliford Ndimbo alisema tayari kikosi cha Kilimanjaro Stars chini ya kocha, Ahmad Ally kimeshawasili Pemba.