Kilimanjaro, Pwani zashinda dhahabu riadha UMISSETA

MIKOA ya Kilimanjaro na Pwani imeshinda medali za dhahabu katika mbio za mita 100 huku Singida na Mara zikishinda mita 1,500 katika michuano ya Umoja wa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) inayoendeleza mkoani Tabora.

Mwanariadha Zahara Shabani kutoka Singida ameshinda mbio hizo akitumia dakika 04:52:73 akifuatiwa na Sarah Lukonza wa Pwani aliyetumia dakika 04:55:53 na nafasi ya tatu ikienda kwa Loicy Manyama kutoka Mkoa wa Mara aliyetumia dakika 04:57:88.

Kwa upande wa mbio za mita 1,500 kwa wavulana mwanaridha Machota Nyamhanga kutoka Mara ameshinda mbio hizo akitumia dakika 04:08:37 huku Mathias Masimba wa Dodoma akishika nafasi ya pili baada ya kutumia dakika 04:09:95 na nafasi ya tatu ikaenda Arusha kwa James Mwatata aliyetumia dakika 04:12:39.

Advertisement

SOMA ZAIDI:https://habarileo.co.tz/wenye-uoni-hafifu-waonyeshana-kazi-umisseta/

Katika mbio za mita 100 kwa wasichana, mwanariadha Martha Andrea kutoka Kilimanjaro ameshinda mbio hizo akitumia sekunde 00:12:60.

Nafasi ya pili imechukuliwa na na majirani zao Arusha, baada ya mwanariadha Jesca Leonard kumaliza mbio hizo akitumia sekunde 00:12:67 na kufuatiwa na Leah Fimbo wa Mwanza aliyetumia sekunde 00:12:87.

Kwa upande wa fainali za mita 100 kwa wavulana, mwanariadha Emmanuel Doto kutoka Pwani ameibuka mshindi baada ya kutumia sekunde 00:10:57 akifuatiwa na Baraka Sanjigwa kutumia sekunde 00:10:96 na Ayoub Nebeth wa Morogoro aliyemaliza nafasi ya tatu akitumia sekunde 00:11:22.

Fainali nyingine ya riadha katika UMISSETA 2024, itaendelea Juni 23 ikihusisha mbio za mita 200, 800, na 100×4 wasichana na wavulana.

Kwa upande wa michezo wa mpira wa mikono, zimechezwa mechi za kumalizia hatua za makundi ambapo kwa wavula Morogoro imeichapa Mwanza mabao 13-11 huku Arusha ikilala kwa Pwani kwa magoli 18-13.