Kilimo tija kuokoa kaya za wakulima Iramba

SINGIDA: MRADI wa NOURISH unaotekelezwa katika mikoa mbalimbali nchini katika kipindi cha mwaka mmoja umefanikiwa kuwainua wakulima wa Iramba kwa kuanzisha bustani za mbogamboga zaidi ya 310, kuunda vikundi 59 vya wakulima vyenye wanachama zaidi ya 1,000 sambamba na kuanzisha mashamba darasa 174.

Aidha, pakti 600 za mbegu za mbogamboga na pingili 39,000 za viazi lishe zimesambazwa kwa wakulima.

Akizungumza katika Siku ya Wakulima wa NOURISH iliyofanyika kijiji cha Ngalagala, Kata ya Kinampanda, Wilaya ya Iramba, Ofisa wa mradi wa NOURISH, Salome James, alisema hayo ni mafanikio mazuri kwa wakulima kwa sababu yamewasaidia kukua na kufanya kilimo chenye tija.

Alisema Shirika la SNV pamoja na Farm Africa kupitia washirika wake RECODA na MIICO wanaendelea kuadhimisha siku ya wakulima wa NOURISH katika wilaya 10 ikiwemo halmashauri ya wilaya ya Iramba, wakilenga kutoa elimu kwa wakulima wanufaika wa mradi pamoja na jamii nzima.

Alisema lengo la maadhimisho hayo ni kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya kilimo na elimu ya lishe, usafi wa mwili na mazingira pamoja na kushiriki katika miradi mbalimbali ambayo itawasaidia wakulima kuongeza kipato, sambamba na fursa ya kujifunza moja kwa moja kutoka kwenye mashamba ya mfano yaliyofanikiwa.

SOMA ZAIDI: Wakulima kupewa elimu cha kilimo tija

Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja wakulima hao wameanzisha bustani za mboga mboga sambamba kupewa pakiti 600 za mbegu za mbogamboga na pingili 39,000 za viazi lishe ili kuwasaidia kulima kilimo chenye tija.

Alisema pamoja na faida hizo pia wakulima hao wameunganishwa na biashara za kilimo, na kuongeza maarifa kupitia mapishi yenye lishe bora.

“Licha ya mafanikio makubwa katika mwaka mmoja, wakulima wamekumbana na changamoto za upungufu wa mvua kutokana na mabadiliko ya tabianchi, pamoja na miundombinu duni ya barabara inayozuia upatikanaji wa pembejeo kwa wakati. Hata hivyo, mradi unaendelea kutoa suluhisho endelevu ili kusaidia wakulima,”alisema Salome.

Alisema mradi wa NOURISH pia umewasaidia wakulima kupima afya ya udongo kwenye mashamba 320, hivyo kuwawezesha kujua ubora wa udongo kwenye mashamba yao.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Afisa Tarafa Charles Makala alisisitiza umuhimu wa wakulima kutekeleza mbinu za kilimo walizojifunza, huku akihimiza maafisa ugani kushirikiana kwa karibu na wakulima ili kuhakikisha teknolojia za NOURISH zinatumika kikamilifu.

“Vikundi vya wakulima, imarisheni ushirikiano,mjisajili rasmi, ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha juhudi zilizowekezwa hazipotei bali zinazaa matunda ya kudumu katika jamii zetu,”alisema Makala.

Maadhimisho ya Siku ya Wakulima wa NOURISH yamefanyika katika wilaya za Momba, Mkalama, Mpwapwa, Sumbawanga, Kalambo, Hanang, na Mbozi na matarajio ni kuendelea kukenga ustahimilivu wa wakulima na kuimarisha sekta ya kilimo kwa maendeleo endelevu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button