Wakulima kupewa elimu kilimo cha tija

MRADI wa Kilimo na Lishe Tanzania (NOURISH -Tanzania), umeandaa siku ya wakulima katika wilaya 10 za mikoa mitano nchini kwa lengo la kuwaelimisha wakulima kuhusu kilimo cha tija ili kuleta mapinduzi kwenye sekta hiyo.

Akizungumza katika kijiji cha Nghumbi, Halmashauri ya Kongwa, mkoani Dodoma, Ofisa wa Mradi wa NOURISH, Theophil Tarimo amesema wamelenga kutoa elimu kwa wakulima wanufaika wa mradi pamoja na jamii nzima ili kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya kilimo.

Alisema katika siku hiyo wakulima watafundishwa elimu ya lishe,kilimo chenye tija, usafi binafsi na usafi wa mazingira pamoja na kushiriki katika miradi mbalimbali ambayo itawasaidia kuongeza kipato.

Alisema mradi huo unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo Norway (Norad) na kutekelezwa na wadau wa maendeleo SNV pamoja na Farm Africa kupitia washirika wake RECODA na MIICO.

Tarimo alisema wilaya 10 zitakazonufaika na elimu hiyo ni za Mikoa ya  mitano ambayo ni Dodoma, Manyara, Rukwa, Singida na Songwe.

Alisema sambamba na hayo wakulima hao watapata fursa ya kujifunza moja kwa moja kutoka kwenye mashamba ya mfano yaliyofanikiwa, kuunganishwa na biashara za kilimo na kuongeza maarifa kupitia mapishi yanayoonesha lishe bora pamoja na burudani za kitamaduni.

Akizungumzia mafanikio ya mradi huo kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita Tarimo alisema: “Mradi wa NOURISH wilayani Kongwa umefanikiwa kuelimisha juu ya wananchi jinsi ya kutengeneza  bustani za nyumbani 177, kuwaunganisha wakulima na kampuni za pembejeo bora za kilimo (mbegu, viatilifu na mashine), kuanzisha vikundi vya kilimo 47 vikiwa na jumla ya wanachama 1,880 pamoja na mashamba darasa 47 na kusambaza miche takribani 28,000 ya viazi lishe.”

Pia kupitia mradi juo wakulima wamepewa pembejeo za kilimo kwenye mashamba darasa na kugawa kilogramu 825 za mbolea ya kupandia na kilogramu 525 ya mbolea ya kukuzia.

Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mayeka Simon ambaye alikuwa mgeni rasmi wa siku ya wakulima wa NOURISH katika halmashauri ya Kongwa alitoa wito kwa wakulima washiriki wa mradi huo kuwa chachu ya maendeleo na watekeleza kwa vitendo kwenye kaya zao yale waliyofundishwa lakini pia kushirikishe wanavikundi wengine elimu hiyo.

“Nashauri serikali za vijiji zihakikishe mmesimamia sheria ndogo ndogo  bila upendeleo ili kuhakikisha maendeleo endelevu ya vikundi na teknolojia zilizoletwa hata baada ya mradi huu kufikia tamati”,alisema Mayeka.

Mradi wa NOURISH ndani ya mwaka mmoja umeleta mafanikio makubwa kwa wakulima zaidi ya 6,000 wameunganishwa na wasambazaji wa pembejeo, watoa huduma 472 wa afya ya jamii wamefundishwa kuhusu lishe bora, na zaidi ya wakulima viongozi 400 wamepata mafunzo ya kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi .

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button