Kilwa Kivinje; mji mdogo historia ‘nzito’

LINDI; KILWA Kivinje ni mji mdogo ulio pembezoni mwa Bahari ya Hindi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi.

Ni mji  uliojizolea sifa kimataifa kwa kuwa mji wa kihistoria unaotambulika na Shirika la Umoja wa Mataifa ya Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Ulipata hadhi hiyo mwaka 1981 kwa kuwa umebeba historia kubwa ya tawala za kikoloni.
Hadi sasa alama zinazobeba historia hiyo zikingali katikati ya mji huo.

Mabaki ya magofu ya kale yameendelea kuwa vivutio katika mji huo yakiwa yanaendelea kushibisha historia hiyo kwa wageni wanaotembelea.

Mhifadhi wa Malikale wa Kituo cha Kilwa Kivinje kutoka Mamlaka ya Uhifadhi wa Wanyamapori (TAWA) wilaya ni Kilwa, Elibariki Petro anabainisha tofauti ya utalii wa malikale katika eneo la Kivinje na Kisiwani au Songo Mnara.

Anasema magofu ya Kivinje yako katikati ya mjini yakiwa yamechangamana na nyumba nyingine za makazi, lakini pia mengine yanaendelea kutumika kwa makazi ya Waswahili (wenyeji) wanaoishi katika mji huo.

Kwa mujibu wa historia, wakati wa utawala wa Zanzibar, Kivinje ilikuwa makao ya liwali wa Sultani kwa Pwani ya Kusini, bandari yake ilikuwa muhimu katika biashara ya utumwa na kulifanya eneo hilo kuwa lango kuu la biashara ya utumwa katika eneo la Kusini.

Tovuti ya ‘Tanzania Tourism’ inaeleza kuwa makadirio ya watumwa walioingia Kivinje kwa mwaka ni watumwa 20,000.
Kwamba waliingia kutoka maeneo mbalimbali ya Kusini kabla ya kusafirishwa kwenda katika masoko makuu kama Zanzibar na Bagamoyo.

Mkazi wa Kilwa Kivinje, Mohamed Mgombela (85) anaelezea Kilwa Kivinje na utajiri wake wa malikale za historia zinazoweza kuvutia wageni hasa watafiri na wanahistoria wanaotembelea kujifunza na kujua historia ya mji huo.

Mwembe Kinyonga
Hilo ni eneo ilipojengwa Hospitali ya Wilaya inayotumika sasa ambako pia kuna Mnara wa Mashujaa wa Vita ya Majimaji.
Mgombela anasema katika eneo hilo wakati huo wa ukoloni kulikuwa na mti mkubwa wa mwembe uliotumika kunyongea mashujaa wa Vita ya Majimaji na ndio asili ya neno hilo la Mwembe Kinyonga.

Jengo la utawala (Boma) lililokuwa na ofisi zote za utawala kuanzia Mkuu wa Wilaya, Mahakama, Magereza, Ofisi ya Kilimo na nyinginezo. (Picha zote na Anna Mwikola)

“Hapa tulipo ni eneo la hospitali ya wilaya ya enzi ya ukoloni,” Mgombela anasema akirejea jengo yalipofanyika mahojiano ambalo sasa limefanyiwa ukarabati kuwa hospitali ya binafsi karibu na Bandari ya kilwa Kivinje.

      Boma la Wilaya
Hili ni boma lililobeba shughuli za utawala wakati wa utawala wa Wajerumani katika eneo la Kivinje.

“Hapo ndiyo palikuwa na ofisi ya DC (Mkuu wa Wilaya). Palikuwa na mahakama, makao ya polisi, makao makuu ya kilimo, yani ofisi zote unazojua wewe za kiwilaya,” anasema.

Mgombela anaongeza, “Kwa hiyo ilikuwa boma, magereza na wizara zote zilikuwa pale.”

Jengo la Bandari ya Kivinje
Kama ilivyoelezwa awali, Kivinje ulikuwa mji wa biashara ya watumwa na bandari yake ilipewa jina la Lango Kuu la Biashara ya Watumwa.

Hapo, kuna jengo lililotumika kama ofisi ya bandari likiwa na ghala la kuhifadhi watumwa waliofika Kivinje kabla ya kupelekwa katika mnada wa watumwa hapo Kivinje.

Soko la Kilwa Kivinje lililotumika kwa minada ya watumwa wakati wa ukoloni, kwa sasa linatumika kuuza bidhaa mbalimbali. (Picha na Anna Mwikola)

Mpaka sasa jengo hilo la ghorofa moja lipo likiwa mkabala na Bandari ya Kivinje inayotumika kusafirisha abiria kwenda katika visiwa vya Songosongo.

Sambamba na jengo hilo la bandari ni jengo la soko la watumwa lililotumika kufanya minada ya watumwa ambalo kwa sasa linatumika kama soko la bidhaa za kawaida.

“Kulikuwa na njia za chini kwa chini kuelekea bandarini. Mtumwa anafungwa kitambaa usoni anazamishwa chini akija akiibuka yuko bandarini,” Mgombea anafahamisha.

Anaongeza: “Anapandishwa kwenye jahazi anapelekwa kwenye masoko makubwa ya Zanzibar na kwengineko.”

Boma kuhamia Kilwa Masoko
Kwa mujibu wa Mgombela, awali makao makuu ya serikali wakati wa utawala wa Wajerumani yalikuwa Kivinje, lakini baada ya Waingereza kuingia na kuchukua madaraka walihamisha shughuli za kiserikali kutoka Kilwa kivinje kwenda Kilwa masoko.

“Sababu ya mkoloni (Mwingereza) kuhamisha boma hapa baada ya kumtoa Mjerumani zamani kulikuwa na boya nje kabisa! Maji hapa ni haba kwa hiyo meli ilikuwa inatia nanga kule mbali, tishali (chombo cha kubeba mizigo kuingiza au kuitoa melini) inabeba mizigo inapeleka kwenye meli au inatoa kwenye meli kuleta bandarini,” anasema.

“Mkoloni akaona suala hili ni zito sana, baada ya utafiti Mwingereza akaona maji Kilwa Masoko ni kina kirefu akaona kwamba kwa usafiri wa bahari ndiyo rahisi kwani anaweza akabeba tani kwa tani, akawaomba wazee wa hapa wenyeji wenye ushawishi, akakaa nao akawaelekeza faida ya bandari,” anasema.

Kwamba, baada ya kuwashawishi na kukubaliana waliamua bandari ihamishwe kwenda Kilwa Masoko, lakini kusingekuwa na tija bila kuanzisha makazi ya watu na shughuli nyingine za kiutawala huko.

“Wakakubaliana, 1948 wakaanza ujenzi wa Kilwa Masoko ndiyo chanzo cha kuhama boma (ofisi za serikali) hapa kwenda masoko, wakalazimisha matajiri wote hapa pamoja na wale wazee kwenda kujenga nyumba Masoko na hiyo ndiyo sababu ya boma kuhamishwa kwenda Masoko,” anaeleza.

Jengo lililotumika kama ofisi za Bandari ya Kilwa Kivinje wakati wa ukoloni. (Picha na Anna Mwikola

“Nadhani na nyie faida yake mnaiona mama Samia (Rais Samia Suluhu Hassan) naye anajenga bandari kubwa ya uvuvi hapo,” anasema.

 Mnara wa Mjerumani
Inaelezwa kuwa, mnara huo unabeba historia ya Mjerumani mmoja aliyeingia Kivinje na msaidizi wake kutafuta mali na kujikuta akiingia mikononi mwa askari wa Mtemi Kinjekitile na kuuawa.

“Palikuja mjerumani mmoja na askari wake mmoja wa Kiswahili wakaweka merikebu yao nje kule wakaja mpaka hapa. Mtemi Kinjekitile aliposikia kwamba kumekuja Mzungu na ameshasimika bendera pale, akaamrisha jeshi lake pale.”

“Mjerumani alipiga risasi mpaka zikamwishia, yule Mswahili akafanikiwa kuingia kwenye merikebu akakimbia,” anasema Mgombela.

Mjerumani huyo alikamatwa na kuuawa kisha kuzikwa kwenye eneo hilo ambalo kwa sasa limepewa jina la Kabungara (Mbunge wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia) Kivinje.

Makaburi ya mashujaa
Makaburi hayo ni mchanganyiko wa makaburi ya mashujaa wa Ujerumani na Waswahili waliopigana Vita ya Majimaji.

Hadithi ya jiwe jahazi

Moja ya hadithi za kushangaza ni hadithi ya jiwe jahazi ambayo Mgombela anaihadithia kuwa kisa chake kinahusiana na Wareno waliotaka kuvamia Kilwa Kisiwani katika karne ya tisa kukutana na vikwazo vya Waarabu.

“Wareno waliingia Kilwa Kisiwani, wakakuta kuna adhana (wito kwa Waislamu kwenda kwenye ibada) karibu 40 ikumbukwe historia inaeleza kwamba Kilwa Kisiwani kulijengwa misikiti 90.”

“Hivyo, walipofika na kusikia adhana hizo wakajiulilza kama waita adhana peke yake wako 40, watakaohitimu 40 maamuma watakuwa wangapi?” anaeleza Mgombela.

Anaendelea kusimulia: “Wakaondoka wakarudi kwenye majahazi yao.”
Kwamba habari zile ziliwafikia Waarabu wakaomba dua majahazi mengine yalifanikiwa kuondoka, lakini moja likabaki na kugeuka jiwe ndiyo mpaka leo unaliona jiwe jahazi,” anaongeza.

Changamoto za uhifadhi
Mgombela anasema changamoto kubwa katika uhifadhi ni uhaba wa elimu ya malikale na umuhimu wake kwa wananchi.
Anasema hali inafanya magofu mengi kuanza kutoweka kwa kuwa kumekuwa na tabia ya watu kuyabomoa.

Anasema: “Changomoto ni ushirikiano kati ya wananchi na wahifadhi wa malikale yaani Tawa kwa sababu malikale inahimiza uhifadhi, lakini wakazi wanabomoa magofu kupata chokaa na matumbawe kujengea.”

“Malikale ihamasishe wananchi, itoe elimu ya uhifadhi,” anahimiza.

Kwa upande wake Petro anasema kumekuwa na wananchi wasio waaminifu wanaobomoa magofu hayo ili kupata vifusi vya matumbawe.

Hata hivyo anafahamisha kuwa, Tawa imekuwa ikifanya juhudi za uhifadhi kwa kuwashirikisha wananchi wenyewe na kuwaelimisha umuhimu wa kulinda mali hizo kwa ustawi wa historia na jamii ya Kivinje.

Kwa mujibu wa Petro, wanafanya juhudi hizo kwa kushirikisha wenyeji wanaoishi kwenye magofu hayo sambamba na wanaoishi kuzunguka magofu hayo.

“Kwa wale wanaoishi tunahakikisha wanayatunza na wale wanaishi jirani na magofu ambayo hayana watu tunahamasisha wayalinde ili yaendelee kubaki,” anasema Petro.

Mmoja wa wakazi katika nyumba hizo za kale ambaye hakutaka jina lake litajwe, anasema ameishi katika nyumba hiyo kwa miaka mingi tangu akiwa na wazazi wake na hapo ndipo nyumbani kwake hivyo ni wajibu wake kupalinda.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button