Desemba 9 kumbukumbu isiyosahaulika

DESEMBA 9, 1961 ni alama isiyosahaulika katika historia ya Tanganyika. Ni siku ambayo ndoto za Watanganyika zilitimia baada ya nchi kujikomboa katika minyororo ya wakoloni ambapo wakati huo alikuwa Muingereza.
Tukio la uhuru wa Tanganyika lilikuwa Desemba 9, 1961, lakini limeendelea kuwa kumbukumbu hata Tanganyika ilipoungana na Zanzibar Aprili 26, 1964 na kuzaliwa kwa jina la Tanzania ambalo ndilo linatumika hadi sasa, lakini tangu wakati huo ikifika Desemba 9 ya kila mwaka, Watanzania wanakumbuka siku hiyo.
Lakini nyuma ya sherehe hizo, kulikuwa na jitihada zisizo na kikomo za viongozi na wananchi wa kawaida, ambao walikuwa na shauku ya kuona Tanganyika ikitawala na kujiongoza yenyewe. Miongoni mwa wapigania uhuru ambao hawataweza kusahaulika katika taifa huru la Tanganyika waliokuwa mstari wa mbele ni hayati Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alikuwa kiongozi wa chama cha TANU (Tanganyika African National Union).

Akizungumza kuhusu mshikamano wa taifa, Mwalimu Nyerere aliwahi kusema: “Hakuna taifa lenye uhuru litakaloendelea bila mshikamano wa wananchi wake.” Katika kipindi hicho aliendelea kuhamasisha wananchi kuondoa ubaguzi wa dini, rangi au kabila, alipenda kuona Watanganyika wote wanashirikiana kwa kushirikisha vijana na wanawake katika harakati za kisiasa, pamoja na kukuza elimu ya uraia na haki za binadamu.
Rashid Mfaume Kawawa na Bibi Titi Mohammed ni miongoni mwa watu waliochukua nafasi muhimu katika harakati i hizi. Kawawa alichangia kwa nguvu katika mipango ya kisiasa na kiutendaji ya TANU, akihakikisha kuwa chama kinalenga ustawi wa taifa.
Bibi Titi Mohammed, aliweka mifumo ya ushiriki wa wanawake, alisema: “Wanawake ni sehemu ya nguvu ya taifa; bila ushiriki wao, hatuwezi kufanikisha uhuru.” Kila kiongozi, kwa nafasi yake, alihakikisha ndoto ya uhuru ilikuwa ndoto ya taifa lote, si ya wachache.

Mchango wa wanasiasa, wanaharakati na wananchi wa kawaida haukufikia kikomo tu katika siasa. Wanawake walihamasishwa kushiriki katika maandamano ya amani, makundi ya elimu ya uraia, na kuchangia katika kampeni za kupigania haki za wananchi. Hii iliunda msingi thabiti wa Tanganyika kujiendeleza baada ya uhuru.
Baada ya jitihada hizi zote, Tanganyika ikapata uhuru wake rasmi Desemba 9, 1961. Lakini uhuru huu haukufikiwa kwa urahisi; ulikuwa matokeo ya mshikamano, kujitolea kwa viongozi walioona mbali zaidi ya maslahi yao binafsi. SOMA: Titi Mohammed: Nguzo ya wanawake katika mapambano ya Uhuru
Uhuru wa Tanganyika ni kumukumbu ya nguvu ya mshikamano wa wananchi, dhamira ya viongozi wa kweli, na thamani ya kujitolea kwa mustakabali wa taifa lote. Ni kumbukumbu inayotakiwa kuenziwa kila mwaka, si tu kwa sherehe bali pia kwa kufundisha vizazi vipya thamani za mshikamano, ushiriki na uwajibikaji wa kila Mtanzania.



