Kinana aipa 5 ACT Wazalendo

Asema ni chama cha hoja sio vihoja

DAR ES SALAAM: CHAMA cha ACT Wazalendo kimepongezwa kwa kuwa chama cha mfano kufanya siasa za hoja na si vihoja.

Hayo yamesemwa leo Machi 5, 2024 na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana akimuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Ufunguzi wa Mkutano wa Taifa wa Chama cha ACT Wazalendo jijini Dar es Salaam.

Amesema “ACT kimekuwa chama cha hoja na si vihoja, tumekuwa tukiwafuatilia, na sisi CCM hatuichukulii ACT kirahisi,”amesema Kinana na kuongeza .

“Kila ilipotokea fursa ya kuunda serikali ya umoja Zanzibar ACT imekuwa tayari mstari wa mbele, kuna wakati  mlipitia kipindi kigumu kidogo mkashusha tanga mkapandisha tanga, halikuwa jambo rahisi mlifanya hivyo bila mifarakano mkafanya kwa umoja na maslahi ya chama chenu,”amesema.

Aidha, Kinana amesema kipindi chama hicho kimeondokewa na kiongozi wake Mkuu Maalim Seif Sharif Hammad ambaye alikua nguzo kuu ya chama hicho baadhi walijiuliza itakuwaje ACT Wazalendo bila Maalim Seif.

“Nahakika wanachama wenu walijiuliza itakuwaje bila Maalim Seif, ila marehemu Seif Sharif Hammad hakujenga mtu alijenga chama, alijenga taasisi, chama chenu kimeendele kuwa imara, nawapongeza viongozi, pia mdogo wangu Zitto Kabwe kwa uongozi madhubuti wenye busara nyingi  na kukiwezesha chama hiki kuwa chama kilichotulia,”amesema Kinana.

Aidha, amesema Zitto amekubali kuzingatia matakwa ya katiba, baada ya vipindi viwili ameamua kukaa pembeni sio kustaafu kwa kuwa  umri wa kustaafu bado.

“Baba wa Taifa ( Mwalimu Julius Nyerere) alipokuwa anaondoka kwenye uongozi wa Urais akabaki kuwa Mwenyekiti wa chama, wapo waliohoji  kwa nini amestaafu Urais lakini bado yupo kwenye Chama?

“Akawajibu ‘before you step down step aside’, naamini Zitto hatokuwa kiongozi lakini atakuwa mshauri mzuri wa chama chake,”amesema Kinana.

Aidha, amempongeza pia Mwenyekiti wa chama hicho, Duni Haji Duni, licha ya kupitia mambo mengi mazuri na mabaya, na mengine mazito ya kuuzunisha lakini amebaki imara ameweka mbele maslahi ya watanzania kuliko maslahi yake binafsi.

Habari Zifananazo

Back to top button