Mgombea amwagiwa sifa, CCM ikizindua kampeni Isimani

IRINGA: Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamezindua kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Isimani kwa kumwaga sifa kwa mgombea wa chama hicho, Emanuela Kaganda Mtatifikolo, wakieleza kuwa anastahili kupewa jimbo hilo
kwasababu ya rekodi yake ya utendaji, uwezo wa kusimamia maendeleo na ukaribu wake kwa wananchi.

Uzinduzi wa kampeni hizo ulifanyika katika Kata ya Itunundu wilayani Iringa Vijijini na kuhudhuriwa na idadi kubwa ya wanachama wa CCM, wafuasi wa chama hicho pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.

Hafla hiyo pia iliwakutanisha wabunge wote wa majimbo ya Mkoa wa Iringa pamoja na wabunge wa Viti Maalumu, walioungana kuonyesha mshikamano wa chama hicho kuelekea uchaguzi huo mdogo.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Salim Asas alisema chama hicho hakijafika Isimani kwa ajili ya kumnadi mgombea kwa maneno ya kisiasa pekee, bali kwa kuamini ana uwezo wa kufanya kazi na kuwaletea wananchi maendeleo.

“Hatujaja Isimani kuja kumnadi tu apewe kura, hapana. Tumekuja hapa kwa sababu tunajua anaweza kuifanya kazi,” alisema Asas.

Alisema Emanuela ni kiongozi mwenye uzoefu mkubwa wa uratibu wa shughuli za chama na maendeleo, akieleza kuwa aliwahi kusaidia kuratibu kampeni katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini zilizohusisha mikoa mitano, zaidi ya majimbo 40 na kata zaidi ya 400.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daud Yasin alisema mgombea huyo ni mnyenyekevu, msikivu na mwenye nidhamu, hivyo akichaguliwa ataweza kusaidia kusukuma mbele maendeleo ya wananchi wa Isimani.

“Ni mnyenyekevu, mtii na anasikiliza. Tukawahimize wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura,” alisema Yasin.

Akizindua kampeni hizo Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Mlezi wa CCM Mkoa wa Iringa, Mohamed Aboud, alisema Emanuela ameonyesha utayari mkubwa wa kuwatumikia wananchi wa Isimani na ana uwezo wa kuendeleza hata kasi iliyoachwa na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, William Lukuvi.

“Emanuela amejipanga kuwahudumia wananchi wa Isimani na ana utayari wa kuongeza kasi ya mtangulizi wake Lukuvi. Ana uwezo mkubwa sana, heshima , nidhamu yake na utayari wake umetuvutia wengi,” alisema Aboud.

Alisema CCM itaendelea kusimamia ajenda ya amani, utulivu na maendeleo ya wananchi, huku akiahidi kuwa changamoto za miundombinu, maji, umwagiliaji, kilimo na mifugo katika jimbo hilo zitapatiwa ufumbuzi kwa kasi zaidi iwapo mgombea huyo atachaguliwa.

Aboud aliwahamasisha wanachama wa CCM kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kuepuka tabia ya kuamini ushindi kabla ya siku ya uchaguzi.

“Kuna kawaida ya kuamini tumeshinda halafu hatuendi kupiga kura. Safari hii tukapige kura kwa wingi tuwaoneshe wenzetu Isimani ni namba moja,” alisema.

Katika hatua nyingine, viongozi waliokuwa wamejitokeza kuwania ubunge kupitia kura za maoni za CCM walionesha mshikamano kwa kuungana kumuunga mkono mgombea huyo.

Aliyekuwa mtia nia wa ubunge jimbo hilo, Arif Abri alisema tofauti za kura za maoni zimekwisha na sasa nguvu zote zinapaswa kuelekezwa kuhakikisha CCM inapata ushindi mkubwa.

“Uchaguzi wa kura za maoni umeisha, sasa tutafanya kampeni. Ushindi wake ni ushindi wa chama,” alisema Abri.

Naye Festo Kiswaga alisema mara baada ya jina la Emanuela kupitishwa na chama, alimpongeza na kusisitiza kuwa makundi ndani ya CCM yamevunjwa.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa CCM Jimbo la Isimani, Emanuela Mtatifikolo, aliwashukuru wana CCM kwa kumuamini na kueleza kuwa amerudi nyumbani kwa lengo la kuondoa hofu iliyojitokeza baada ya kuondoka kwa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo.

“Wana Isimani, mimi mtoto wenu nimerudi. Mimi ni mtendaji zaidi na ninapenda matokeo,” alisema.

Emanuela alisema sekta za kilimo, maji, afya na miundombinu ni miongoni mwa maeneo atakayoyapa kipaumbele, akiahidi kusukuma utekelezaji wa miradi mikubwa ya barabara na kuongeza uzalishaji wa mpunga katika eneo la Pawaga.

“Mchele wa Pawaga utajulikana kimataifa. Ili kuufikisha sokoni tunahitaji barabara ya Pawaga-Iringa Mjini pamoja na miundombinu mingine muhimu,” alisema.

Uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Isimani unafanyika kufuatia aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo William Lukuvi kufafiki dunia hivi karibuni, hali iliyosababisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutangaza nafasi hiyo kuwa wazi na kuitisha uchaguzi mdogo.

Mbali na CCM, jumla ya vyama 17 vya upinzani vimejitokeza kushiriki uchaguzi huo, huku macho na masikio ya wananchi yakisubiri kuona namna vyama hivyo vitakavyozindua kampeni zao katika harakati za kuwania jimbo hilo muhimu la Mkoa wa Iringa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button