Kiruswa ataka wananchi waelimishwe hewa ukaa

LONGIDO: NAIBU Waziri wa Madini na Mbunge wa Jimbo la Longido mkoani Arusha, Dk. Stephen Kiruswa, ameitaka Kampuni ya Soils for the Future Tanzania kutoa elimu zaidi kwa wananchi kuhusu mradi wa hewa ukaa ili kuondoa hofu na dhana kuwa mradi huo una malengo mabaya kwa jamii.
Kiruswa alitoa kauli hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Lesing’ita, Kata ya Mundarara, Wilaya ya Longido, baada ya baadhi ya wananchi kueleza wasiwasi kuhusu mradi huo, wakidai kuwa ardhi imeuzwa, mradi umesainiwa na watu wachache na elimu ya kutosha haikutolewa kwa jamii kabla ya utekelezaji wake.

Alisema mradi wa hewa ukaa ni muhimu kwa wananchi wa Kata ya Mundarara na Longido kwa ujumla, hivyo ni muhimu jamii kupata uelewa wa kutosha kuhusu malengo yake na manufaa yanayotarajiwa.
Aliongeza kuwa Serikali Kuu na Chama Cha Mapinduzi (CCM) vinatambua umuhimu wa mradi huo, akieleza kuwa waendelezaji wake walipata baraka kutoka Serikali Kuu.
Naibu Waziri huyo alisema idadi ndogo ya wananchi walioshiriki katika vikao vya awali vya kujadili na kupitisha mradi huo ni miongoni mwa mambo yanayohitaji kufanyiwa kazi ili kuhakikisha jamii nzima inapata nafasi ya kuelewa na kushiriki katika maamuzi yanayohusu maendeleo yao.
Kutokana na hali hiyo, Kiruswa aliiagiza kampuni hiyo kuitisha kikao kingine Novemba 7, mwaka huu, kikihusisha viongozi wote wa serikali na chama, viongozi wa kimila, watu maarufu na wananchi wengine, wakiwemo yeye mwenyewe, ili kujadili mradi huo na kufikia muafaka unaozingatia maslahi ya wana Longido.
Alisema ushiriki mpana wa wananchi ni muhimu katika kuondoa sintofahamu iliyojitokeza na kuhakikisha kuwa jamii inapata ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa mradi huo, badala ya kuendelea kuwepo kwa hofu na madai yanayoweza kuongeza mvutano miongoni mwa wananchi.
Akizungumzia suala la makundi ndani ya jamii na chama, Kiruswa alisema tofauti zilizoanza wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka jana zimeendelea kujenga uhasama kati ya baadhi ya wananchi na viongozi waliochaguliwa.

Aliahidi kukutana na waratibu wa makundi hayo ili kujadili changamoto zilizopo na kutafuta muafaka utakaosaidia kurejesha mshikamano na ushirikiano katika jamii ya Longido.
Kiruswa alisema makundi ndani ya chama yanaweza kuwa kikwazo kwa maendeleo iwapo yataendeleza migawanyiko badala ya kuunganisha wananchi katika shughuli za maendeleo.
Alisema, akiwa Mbunge wa Jimbo la Longido, atahakikisha anaitisha vikao mapema iwezekanavyo mwishoni mwa mwezi huu ili kujadili tofauti hizo na kuhakikisha kila mmoja anaheshimu maamuzi ya wananchi waliochagua viongozi waliopo madarakani.
Alisisitiza kuwa ni muhimu wananchi na viongozi kuweka mbele maslahi ya jamii na maendeleo ya eneo hilo, huku wakitafuta njia za kumaliza tofauti zao kwa mazungumzo.
Kwa upande wake, Meneja wa mradi wa Kampuni ya Soils for the Future Tanzania, Richard Ndasikoi, alimshukuru Kiruswa kwa kutoa ufafanuzi kwa wananchi wa Kata ya Mundarara kuhusu uhalisia wa mradi huo.
Ndasikoi alisema ufafanuzi huo utasaidia kuondoa dhana iliyoenezwa na baadhi ya watu kuwa kampuni hiyo imechukua ardhi yote katika kata hiyo, akisisitiza kuwa madai hayo si ya kweli.
Alisema kampuni iko tayari kutoa elimu zaidi kwa kushirikisha jamii nzima, kama alivyoagiza mbunge huyo, ili kuhakikisha wananchi wanapata uelewa mpana kuhusu malengo ya mradi na manufaa yake.
Aliongeza kuwa lengo la kampuni hiyo ni kuhakikisha jamii inafahamu kwa kina mradi huo na nafasi yake katika kuleta manufaa kwa wananchi wa Longido.
Naye Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Chama Mwita, aliwataka wananchi wa Kijiji cha Lesing’ita, Kata ya Mundarara na maeneo mengine kujitokeza kwa wingi katika kikao kilichopangwa kufanyika Novemba 7, mwaka huu.

Mwita alisema ushiriki wa wananchi ni muhimu katika kujadili na kufikia muafaka kuhusu mradi huo ili jamii iweze kuelewa namna itakavyonufaika nao.
Aliongeza kuwa wananchi wanapaswa kupata taarifa sahihi kuhusu mradi huo na kuepuka kueneza madai yasiyothibitishwa ambayo yanaweza kuongeza hofu na mvutano ndani ya jamii.
Alisema mradi wa hewa ukaa unasimamiwa na kuratibiwa na Serikali Kuu, akieleza kuwa sera na mipango ya serikali inatambua umuhimu wa miradi ya aina hiyo.
Mwita alisisitiza kuwa ardhi ni ya wananchi na kwamba masuala yanayohusu matumizi yake yanapaswa kufafanuliwa kwa uwazi ili wananchi waweze kuelewa taratibu zinazotumika na namna maslahi yao yanavyolindwa.



