Kishindo Benki ya Ushirika

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema ndoto imetimia ya kuwa na Benki ya Ushirika nchini na imeanza ikiwa imara.
Benki hiyo imeanzishwa kwa kuziunganisha Benki ya Ushirika ya Kilimanjaro (KCBL) na Benki ya Wananchi ya Tandahimba (TACOBA).
Akizindua benki hiyo Dodoma, Rais Samia amesema uanzishwaji wa benki hii si wa bahati mbaya, bali ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 – 2025 na mawazo yaliyokuwepo kwa muda mrefu.
Alisema safari ya uanzishwaji wa Benki ya Ushirika ingeweza kuwa mapema, lakini ilikwamishwa na upatikanaji na mitaji ya uhakika na kusisitiza kuwa muundo wa umiliki wa benki hiyo ni kielelezo cha nguvu za ushirika wa sasa.
Alisema muundo huo unalenga usimamizi wa kitaalamu na uendelevu wa kifedha na huduma jumuishi kwa makundi yote yale ambayo yalikuwa hayafikiwi.
Rais Samia alisema amepata matumaini kuona kuwa benki hiyo haijaanza kinyonge, kwani imeanza na mtaji wa Sh bilioni 58, kiasi cha fedha ambacho kinatakiwa upatikanaji wa mitaji ili kuongeza tija kwa kilimo, kuhakikisha usalama wa chakula na kuchochea maendeleo vijijini.
“Ni matarajio yetu kuwa kila Shilingi inayowekezwa na benki hii kwenye ushirika na kilimo itavutia na kuchagiza taasisi nyingine za fedha kuongeza kiwango wanachokielekeza kwenye sekta ya kilimo,” alisema Rais Samia.
Aidha, alipongeza hatua ya benki hiyo kuanza ikiwa na matawi manne, mawakala 58 na maelfu ya wateja, na kusisitiza kuwa hatua hiyo inaonesha kuanza kwa kishindo na kukubalika kwa haraka.
“Inatoa moyo kuona mmejipanga kuhakikisha huduma zenu zinafika kwa walengwa wote, kwa urahisi na kwa gharama nafuu. Ubunifu wa utumiaji au kutumia ofisi zote za vyama vikuu vya ushirika na SACCOS (Vyama vya Akiba na Mikopo) ili kufikia wananchi wa kipato cha chini na walio vijijini kwenye vikundi vya kijamii, wakulima na wafanyabiashara wadogo, ni hatua nzuri ya kuanzia,” alisema Rais Samia.
Aliongeza: “Hivyo nitoe rai kwa vyama vya ushirika kushirikiana na Benki ya Ushirika kupanua mtandao wake ili
huduma zifike na kupatikana kwa urahisi”.
Alisema kwa mujibu wa taarifa za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) za mwaka 2023, fedha zinazoelekezwa kwenye sekta ya kilimo ilikuwa ni asilimia 10 ya mapato hivyo kufikia Azimio la Afrika.
Alisema kumekuwa na kasi ndogo ya kuongezeka kwa mitaji katika sekta ya kilimo ikilinganishwa katika sekta nyingine, hivyo kuwepo kwa Benki ya Ushirika kutaongeza upelekekaji wa mitaji kwa wakulima na sekta nzima
ya kilimo.
Amesisitiza uzingatiaji wa misingi iliyowekwa na BoT katika uendeshaji wa benki ili kuihakikishia uimara, uwezo wa kujiendesha kibiashara na uendelevu wake.
Pia, ameziomba benki nyingine kushirikiana na benki hiyo ya ushirika ambayo imekuja si kuongeza ushindani, bali kusaidia kuongeza nguvu na njia za kuwafikia Watanzania hasa wa vijijini.
Rais Samia alisema dhamira ya serikali ni kuona ushirika unachukua nafasi yake ili iongeze tija kwenye kilimo na kuongeza mchango kwenye Pato la Taifa.
Alisema serikali imechukua hatua za makusudi kuisaidia sekta ya kilimo ili kuongeza uzalishaji, kuongeza usalama wa chakula na kukuza kilimo biashara, na pia kuifanya sekta ya kilimo ikue kwa asilimia 10 ili ichangie Pato la Taifa zaidi ya asilimia 26 inayochangiwa sasa kwa takwimu za mwaka jana.
Alisisitiza maeneo matatu ya kuyatilia mkazo ikiwamo Tume ya Maendeleo ya Ushirika kujenga ushirika imara utakaofanya mambo makubwa wenyewe.
“Kwa watu ambao hawakuwa na imani na ushirika, mimi (Rais Samia) nilikuwa mmojawapo, nilikuwa naona ushirika ni chaka la wizi, ushirika ulikuwa na sifa mbaya, lakini sasa umesimama vizuri kiasi ambacho unazidi kunipa hamu ya kuendelea kusaidia maendeleo ya ushirika nchini,” alisema Rais Samia.
Ameitaka kuwa wabunifu kwa kutanua wigo wa huduma zao, kuhamasisha wanaushirika kujiunga kwenye mfuko, kuangalia namna ya kuwaunganisha wakulima na mifuko ya hifadhi ya jamii ili kuongeza ustawi wao.
Pia, amevitaka vyama vya ushirika kujiendesha kibiashara na kwa uwazi kwa kutoa taarifa za fedha kwa wakati hali itakayoongeza imani kwa wanaushirika na wauone ushirikia ni eneo litakalowainua kiuchumi.
Pia, amevitaka vyama vya ushirika kutumia mifumo ya Tehama na taarifa za ziwasilishwe kwa wakati, amewahakikishia wanaushirika na benki hiyo kuwa serikali itahakikisha ushirika unaleta maendeleo ya kweli kwa jamii ya Watanzania.
Ameiagiza Wizara ya Kilimo kuiangalia sekta ya ushirika na kuhamasisha wakulima wajiunge kwenye ushirika ili kunufaika na fursa za mitaji na kujiimarisha kiuchumi.
Rais Samia pia ameagiza Wizara ya Fedha, Kilimo na BoT kukutana na kuzungumza ili kuja na mfumo kiongozi
kuondoa ombwe la mikopo katika sekta ya kilimo.
Pia, ameagiza fedha kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) iende kwenye mfuko wa pembejeo na benki hiyo ili
kufungua madirisha maalumu kwa wakulima na kuhakikisha wanakopesheka na mitaji inaongezeka na mazao yanaongezwa thamani.