Kishindo Mkutano Mkuu CCM leo

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan akiongoza Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kilichofanyika jijini Dodoma Januari 18. (Picha na Ikulu)

WAJUMBE wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo wanaanza kikao chao cha siku mbili ambacho pamoja na mambo mengine wanakwenda kupiga kura ya kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara.

Nafasi hiyo iliachwa wazi na Abdulrahman Kinana aliyeandika barua ya kujiuzulu wadhifa wake kwa Rais Samia Suluhu Hassan Julai, mwaka jana.

Mbali na kujaza nafasi hiyo, pia mkutano mkuu huo utakuwa na kazi ya kupokea taarifa ya chama kuanzia mwaka 2022 hadi 2025 na kupokea taarifa ya utekelezaji Ilani ya Uchaguzi ya CCM kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

Advertisement

Mkutano huo umetanguliwa na vikao vya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) ambavyo vimefanyika Ikulu ya Chamwino na kuongozwa na Mwenyekiti wa chama, Rais Samia Suluhu Hassan.

Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa pamoja na mambo mengine kilikuwa na kazi ya kujadili jina la anayependekezwa kushika nafasi ya Makamu Mwenyekiti na kisha mapendekezo hayo yamefikishwa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM ambayo italiwasilisha kwa wajumbe wa mkutano mkuu kwa ajili ya kupigiwa kura ya ndiyo au hapana.

Maandalizi ya mkutano huo yanaonekana kukamilika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma. Mji umepokea idadi kubwa ya wajumbe huku bendera za CCM zikipepea jijini.

Atakayechaguliwa kushika wadhifa huyo atakuwa kada wa CCM wa sita kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara chini ya utaratibu ulioanza baada ya mfumo wa vyama vingi.

Waliowahi kushika wadhifa huo ni Rashid Kawawa, John Malecela, Pius Msekwa, Philip Mangula na Kinana.