Kitendawili jakuzi la Sh mil 6 nyumba ya mkurugenzi

KIGOMA: WAJUMBE wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) Mkoa wa Kigoma wamehoji uhalali wa Halmashauri ya Wilaya Kigoma kiasi cha Sh milioni 6.5 kuweka Jakuzi la kuogea kwenye nyumba ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo wakati halmashauri inachangamoto kubwa ya fedha katika utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Hali hiyo imetokea wakati wajumbe hao waliokuwa na kikao cha kawaida cha jumuiya hiyo kwa Mkoa wa Kigoma walipotembelea kuangalia maendeleo ya utekelezaji wa baadhi ya miradi ya halmashauri hiyo ikiwemo nyumba hiyo ya Mkurugenzi Mtendaji.

Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Kigoma,Jacskon Mateso aliuliza watendaji wa halmashauri hiyo waliokuwa wakiongoza ziara hiyo kwamba halmashauri ilizingatia nini kuweka Jakuzi hilo kwa bei hiyo wakati bado halmashauri inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uhaba mkubwa wa nyumba za watumishi.

Wakiwa katika eneo hilo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Kigoma, Exavery Ntambala alitoa taarifa kuwa nyumba hiyo ya Mkurugenzi na nyumba nyingine ya watumishi iliyopo kwenye eneo hilo zimejengwa kwa gharama ya Sh milioni 270 na jakuzi kwenye nyumba ya mkurugenzi imegharimu zaidi ya Sh milioni sita.

Ntambala alisema kuwa nyumba hizo mbili ni sehemu ya nyumba za watumishi 19 zinazohitajika na kutokana na uhaba wa fedha halmashauri imeweza kujenga nyumba hizo mbili hivyo inatafuta fedha kujenga nyumba nyingine 17.

Diwani wa viti maalum Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, Asha Omari alisema kuwa hayo ni matumizi mabaya ya fedha za serikali wakati halmashauri ina mzigo mkubwa wa kugharamia miradi mbalimbali ya wananchi huku fedha nyingi zinatumika kujenga kitu kimoja cha anasa bila sababu.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button