THRDC, Wamasai waungana kulaani mauaji ya Bhaozang Ge

DAR ES SALAAM: WAKILI wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa, ameliomba Jeshi la Polisi kushirikiana na viongozi wa jamii ya Kimasai jijini Dar es Salaam ili kubaini watu wanaodhaniwa kuhusika katika mauaji ya raia wa China ambaye ni mmiliki wa kiwanda cha kuchakata chupa za plastiki, Bhaozang Ge.
Olengurumwa amesema hatua hiyo itasaidia kurejesha imani ya jamii kwa watu wa kabila hilo, baada ya baadhi yao kudai kuanza kukumbwa na changamoto za kijamii na kupoteza ajira kufuatia tukio hilo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wanajamii wa Kimasai, Olengurumwa amesema ni muhimu uchunguzi wa kina ufanyike ili kubaini wahusika halisi badala ya jamii nzima kuhusishwa na tukio hilo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Wamasai jijini Dar es Salaam, Elia Sangeti Taiko, amesema jamii hiyo inalaani tukio hilo na ipo tayari kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuwabaini waliohusika.
“Tunalaani aliyefanya tukio hilo kwa ndugu yetu Mchina. Tumekuja kuonana na wakili ili atutetee na atukutanishe na Jeshi la Polisi kwa sababu aliyefanya kitendo hicho ni mtu mmoja na sio jamii nzima ya Wamasai,” amesema Taiko.
Amesema tukio hilo limeathiri mahusiano kati ya jamii ya Wamasai na waajiri wao, huku baadhi yao wakikumbana na unyanyapaa katika maeneo ya kazi na biashara.

Naye katibu wa umoja huo, Laizer Lobulu, ameliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina na kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake dhidi ya mtuhumiwa atakayebainika, bila kuihusisha jamii nzima ya Kimasai.
“Sasa hivi tukipita tunaitwa wauaji kwa sababu ya mtu mmoja anayedaaiwa kuwa ni Masai. Kwakweli tunakerwa sana kuitwa wauaji kwa kosa la mtu mmoja,” amesema Lobulu.
Aidha, Lobulu amewataka waajiri kuwa na utaratibu wa kutambua vizuri taarifa za waajiriwa wao, ikiwemo kuwa na wadhamini, ili kusaidia endapo kutatokea matukio ya kihalifu.
Katika hatua nyingine, Mjumbe wa umoja huo, Julius Singoi, amewataka Wamasai wote waliopo jijini Dar es Salaam kuhudhuria kikao kitakachofanyika siku ya Jumapili katika eneo la Mabibo, akisema kutakuwa na ushirikiano na Jeshi la Polisi na hakuna sababu ya hofu.
Ikumbukwe kuwa Bhaozang Ge alifariki dunia Mei 16, 2026 kwa kuuawa na mwili wake kutupwa kwenye mtaroni na wanaodaiwa kuwa ni walinzi wa kiwanda hicho



