Kitila: Hakuna sababu ya kuagiza nondo, mabati nje

SERIKALI imesema hakuna haja ya kuagiza nondo na mabati kutoka nje ya nchi kwa sababu viwanda vilivyopo nchini vinakidhi mahitaji.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema hayo alipotembelea kiwanda cha Lodhia wakati wa ziara ya kutemebelea viwanda wilayani Mkuranga.
Profesa Kitila amesema hadi sasa kuna viwanda 19 vya kuzalisha nondo na vinne vya kuzalishabati nchini ambavyo kwa pamoja vinakidhi mahitaji.
“Kama nchi, sasa hatuna sababu ya kuagiza nondo kutoka nje hii ni habari njema hivyo mahitaji muhimu ya nchi tunaweza kuyakidhi,” alisema.
Profesa Kitila alisema mahitaji ya nondo nchini ni tani 600 kwa mwaka na viwanda vilivyopo vinazalisha takribani tani 1,200.
Pia, alisema serikali ina wajibu wa kuvilinda viwanda vya ndani kwa kuwatengenezea mazingira rafiki ya uwekezaji pamoja na kuzui uingiaji holela wa bidhaa kutoka nje.
Profesa Mkumbo amehimiza Watanzania watumie bidhaa zinazozalishwa nchini katika kutekeleza miradi.
Mwenyekiti wa wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mariam Kisangi ameipongeza serikali kwa dhamira yake ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uwekezaji.
Kisangi alisema wameridhika kuona uwekezaji wa viwanda unavyofanyika nchini na kuahidi kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili ikiwemo ya umeme wa uhakika pamoja na uingizwaji wa bidhaa kutoka nje ili kulinda viwanda vya ndani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Lodhia, Manoj Gopi alisema uwekezaji uliofanywa katika kiwanda hicho ni Dola za Marekani milioni 102 na kimetoa ajira kwa watu 2,370.
Gopi alisema kiwanda hicho kinahudumia soko la ndani kwa bidhaa za nondo, mabati na mabomba. Nyingine zinauzwa katika nchi za Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Meneja wa Huduma za Uwekezaji Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) James Maziku alisema kiwanda cha Lodhia ni
miongoni mwa uwekezaji wa kimkakati nchini.
Maziku alisema kiwanda hicho kilianza kwa mtaji mdogo na kwa sasa kimezidi kukua kutokana na mazingira rafiki ya uwekezaji.
Katika ziara hiyo, Profesa Kitila alifuatana na wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam lengo likiwa ni kusikiliza changamoto za wamiliki wa viwanda na kuonesha umma mchango wa viwanda katika uchumi wa nchi.



