Kiwango cha umaskini chapungua

WAZIRI  wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba  amesema Tanzania imefanikiwa kupunguza kiwango cha umasikini uliokithiri kutoka asilimia 9.7 kwa mwaka 2011/12 hadi asilimia 8.0 mwaka 2017/18.

Mwigulu ameyasema hayo leo Juni 15, 2023 akiwasilisha  Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 Bungeni Jijini Dodoma.

Amesema utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya wa mwaka 2017/18 ulionesha kuwa asilimia 26.4 ya Watanzania walikuwa wanaishi chini ya mstari wa umasikini wa mahitaji ya msingi, hali hiyo imepungua kutoka asimilia 28.2 kwa mwaka 2012.

“Tanzania imefanikiwa kupunguza kiwango cha umasikini uliokithiri kutoka asilimia 9.7 kwa mwaka 2011/12 hadi asilimia 8.0 mwaka 2017/18,”amesema Mwigulu na kuongeza

“Hata hivyo, kiwango cha umasikini kimeendelea kupungua lakini siyo kwa kasi ya kuridhisha hivyo bado kuna Watanzania masikini.”Amesema

Amesema,  licha ya kiwango hicho cha umaskini kupungua, pamoja na utajiri uliopo nchini, na hatua kubwa iliyopigwa hata hivyo  bado kuna wananchi maskini.

“Kiwango cha umasikini cha mahitaji ya msingi kitaifa kinapimwa kwa kuangalia Wanakaya wanaoishi kwa kutumia chini ya shilingi 49,320 kwa mwezi kwa Mtu mzima kwa ajili ya kupata mahitaji ya msingi.

“Vilevile, kiwango cha umasikini uliokithiri (umasikini wa chakula) unapimwa kwa kuangalia Wanakaya wanaoishi kwa kutumia chini ya shilingi 33,748 kwa mwezi kwa mtu mzima hivyo kushindwa kumudu kupata chakula chenye kalori 2,200 zinazotakiwa kwa mtu mzima kwa siku.

Habari Zifananazo

Back to top button