Besigye afikishwa mahakama ya jeshi

UGANDA : MWANASIASA mkongwe wa Uganda Kizza Besigye na mshtakiwa mwenzake, Obeid Lutale wamefikishwa katika mahakama ya kijeshi mjini Kampala, huku kukiwa na ulinzi mkali.
Wawili hao wanakabiliwa na mashtaka manne yakiwemo ya kumiliki silaha kinyume cha sheria, tuhuma ambazo wamekanusha dhidi yao.
Wakati huo huo baraza la sheria la Uganda lilimyima kibali Martha Karua ambaye ni waziri wa zamani wa sheria wa Kenya ambaye alipangwa kuongoza timu ya mawakili wa Besigye.
Baraza hilo pia lilidai kuwa maombi ya Martha Karua kuongoza timu hiyo yana uchochezi wa kisiasa kuliko ya kitaaluma. SOMA: Martha Karua kumtetea Besigye
Hata hivyo, Martha ameapa kuendelea kuhudhuria kesi ya mahakama ya Besigye akiahidi pia kuiunga mkono timu hiyo ya wanasheria kwa uwezo wowote hata kama sio kama wakili wake.
Kiongozi huyo wa upinzani alitekwa nyara alipokuwa ziarani nchini Kenya mwezi uliopita na kupelekwa kwenye gereza la kijeshi nchini Uganda.
Hatua hiyo ilizua shutuma nyingi na hofu ya mabadilishano ya siri ya taarifa za kijasusi kati ya mataifa hayo mawili jirani.



