KKKT kuwainua mabinti waliopata mimba

DAR ES SALAAM; Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, limesema linaimarisha ushirikiano na Serikali pamoja na wadau wengine kusaidia wasichana wanaopata mimba katika umri mdogo kurejea katika masomo na kutimiza ndoto zao.

Kauli hiyo imetolewa na Msaidizi wa Askofu wa Dayosisi hiyo, Dean Chediel Lwiza, wakati wa uzinduzi wa huduma ya Binti Mama katika Usharika wa Manzese, Jimbo la Kaskazini, jijini Dar es Salaam.

Huduma hiyo itatekelezwa katika Wilaya za Ubungo na Temeke, ikilenga kuwasaidia wasichana waliopata watoto katika umri mdogo kupitia ushauri nasaha, uwezeshaji wa kiuchumi na elimu ya malezi ya watoto.

Maafisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa za Temeke na Ubungo, Neema Mambosho na Jackline Malya, wamesema huduma hiyo imekuja wakati mwafaka kutokana na ukubwa wa changamoto ya mimba za utotoni katika jamii, huku wakitaja malezi kuwa mojawapo ya maeneo yanayohitaji kupewa kipaumbele.

Kwa upande wao, wachungaji walioshiriki uzinduzi huo, akiwemo Kaimu Mkuu wa Jimbo la Kaskazini, Mchungaji Ibrahim Munanka, Jane Kamugisha na Rose Machui, wamehimiza kuendelea kutolewa kwa elimu ya kujikinga na mimba za utotoni ili kupunguza tatizo hilo.

Mratibu wa Diakonia wa Dayosisi hiyo, Anna Nyumba, amesema huduma hiyo inalenga kuwajengea wasichana ujasiri na kuwapa msaada wa kukabiliana na changamoto zinazoweza kuwazuia kufikia malengo yao.

Mradi huo utatekelezwa kwa miaka miwili na unatarajia kuwafikia wasichana 100 katika Wilaya za Ubungo na Temeke.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button