Klabu kupinga rushwa shuleni ziwe msingi wa Tanzania bora

TANZANIA imejipambanua kuwa miongoni mwa nchi zinazopiga vita rushwa kwa nguvu zote katika ngazi zote za maamuzi na huduma. Rushwa nchini Tanzania ni adui wa haki.

Kwa miaka kadhaa, shule za msingi, sekondari na vyuo nchini zimeanzisha klabu za kupinga rushwa, hatua inayohitaji nguvu ya pamoja kuleta tija kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Hivi karibuni wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Dk Samia na Bunge za mkoani Dodoma walipongezwa kutokana na mdahalo mzuri waliofanya kuhusu rushwa inavyoathiri uchaguzi mkuu katika maeneo mbalimbali nchini.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Ismail Ally Ussi wakati wanafunzi hao waliposhiriki mdahalo uliofanyika katika Shule ya Msingi Mtemi Mazengo iliyopo Kata ya Ipagala,

Jiji la Dodoma aliwasifu wanafunzi hao kwa kuonesha uelewa mkubwa kuhusu madhara ya rushwa. Uwezo waliyouonesha wanafunzi hao wa kujadili masuala ya rushwa unadhihirisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) inafanya kazi kubwa kwa vijana na wanafunzi kuhusu madhara ya rushwa.

Kwanza, tunaipongeza Takukuru na serikali kwa uwekezaji huu kwa wanafunzina vijana kwani ni wazi klabu za rushwa mashuleni zinalenga kuwajengea wanafunzi misingi imara ya kuchukia na kukataa vitendo vya rushwa angali wadogo.

Tunaamini misingi hii ikiwa imara, tutajenga kizazi cha Watanzania wanaochukia rushwa tangu utoto wao na hivyo
kuwa na taifa imara na lenye mgawanyo wa haki wa rasilimali zake.

Hivi sasa tunaona juhudi zinazofanywa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika mapambano dhidi ya rushwa. Kauli zake, elimu kwa jamii, mabango, vipeperushi katika ofisi za umma, barabarani na maeneo ya huduma kama afya, maji na umeme vinadhihirsha nia ya dhati ya serikali kutokomeza rushwa.

Tunawashauri wanafunzi walio katika klabu hizi kuongeza bidii kupambana na janga hili kwa kufanyia kazi elimu wanayoipata ili watakaposhika nafasi za uongozi waweze kutenda haki na kusimamia kanuni, taratibu na sheria.

Tunashauri shule na vyuo vikuu na klabu hizi vizianzishe mara moja na zile zenye klabu ziziimarishe zaidi ili kujenga kizazi imara cha wapinga rushwa wasiotikiswa wala kuyumbishwa.

Hakuna asiyefahamu madhara ya rushwa kwani wapo waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki kwasababu walikosa hela ya kuhonga ili ndugu zao watibiwe, wapo waliokosa masomo, kazi kwasababu ya rushwa, hivyo adui huyu si wa kada fulani bali ni wa taifa zima.

Tunasisitiza serikali iwekeze zaidi katika klabu hizi kujenga nchi bora. Tunaamini Tanzania bila rushwa inawezekana kila mtu akitekeleza wajibu wake na kuikataa kwa maneno na vitendo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button