Komandoo Salmin, Dk Shein wasisitiza usiri vikao CCM

ZANZIBAR: RAIS Mstaafu wa Zanzibar Dk Salmin Amour Juma amewataka viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukisimamia vyema chama hicho, huku akionya usiri wa vikao vya chama lazima uzingatiwe.

Salmin maarufu kama Komandoo, ametoa kauli hiyo alipotembelewa na Katibu Mkuu wa CCM,  Dk. Emmanuel Nchimbi, ambaye pia alimtembelea Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na wazee wa CCM kwenye mikutano yao ya mabaraza, Pemba na Unguja.

Akizungumza Dk Salmin ambaye hajaonekana hadharani kwa muda mrefu, amesema amefarijika kutembelewa na Katibu huyo wa CCM Bara na kusema: “Asanteni. Waambie pia nawasalimia. Simamieni chama…chama kijengwe, kisimamiwe kupata ushindi mzuri.”

Kwa upande wa Dk. Shein, amesisitiza umuhimu wa CCM kuendelea kusimamia misingi ya kuanzishwa kwake.

“CCM ni chama makini sana. Kina misingi na taratibu zake. Na jambo zuri ni kwamba Katibu Mkuu ndiye msimamizi. Nakujua, tumekuwa wote Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa muda mrefu. Sina shaka nawe kuyasimamia haya. “Tukipindisha taratibu tutaanza kwenda kombo. Jengine ni suala la usiri wa vikao, lazima vikao viwe na siri,” amesema Dk. Shein.

Kwa upande wake, Balozi Nchimbi amesema ushauri na maelekezo ya viongozi wastaafu wa chama na serikali, pamoja na wazee wa CCM kuhusu umuhimu wa kuendelea kukiimarisha chama, ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwatumikia watu vizuri, yatafanyiwa kazi kwa uzito unaostahili.

Habari Zifananazo

Back to top button