Kongamano kuhamasisha maendeleo ya wanawake

GEITA: Benki ya Stanbic Tanzania imedhamini Kongamano la Maendeleo ya Wanawake katika Halmashauri ya Ushirombo mkoani Geita ikiwa sehemu ya kuelekea kilele cha Wiki ya Wanawake.
Akizumgumza kwenye kongamano hilo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima amesema kongamano hilo maalumu linalengo la kuhakikisha kuwa maendeleo ya wanawake yanapewa msukumo unaostahili katika taifa.
Aidha, Waziri Dorothy amesema kuwa moja ya malengo yao makuu ni kuona wanawake wanapewa fursa zote za kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa.
“Katika muktadha huu, tunatazama nyuma kuona tulipotoka, lakini muhimu zaidi, tunajikita kwenye mwelekeo wa mbele kuhakikisha kuwa wanawake wanapewa fursa zote za kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa taifa letu,” alisema waziri.
Kongamano hilo maalum lililofanyika mkoani Geita Jumapili lililenga kutambua mchango wa wanawake wa mkoani humo na Tanzania kwa ujumla katika maendeleo ya taifa.

Kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, kitaifa yanatarajiwa kufanyika mkoani Arusha na kuongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Pia waziri huyo aliishukuru benki ya Stanbic kwa kufanikisha kongamano hilo na kutoa wito kwa mabenki mengine nchini kuiga mfano wao.
Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Idara ya Biashara wa Stanbic Tanzania, Fredrick Max, amesema azma yao ni kuunga mkono jitihada za serikali katika kuwainua wanawake.
“Jambo hili ni jukumu letu sote, serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo. Sisi Benki ya Stanbic tunatekeleza azma hii kwa vitendo kwa kutoa mikopo nafuu tukijikita kuwawezesha wanawake na vijana kiuchumi,” amesema.
Kwa kuongezea Max alisema kuwa kuonesha kuwa safari ya maendeleo ya wanawake wanaozingatia zaidi wameweza kuwa na progamu maalum, kama programu ya Ignite women au “kuwasha wanawake” ambao umelenga kuwawezesha wanawake kuwa na uwezo wa kuongoza na kujiamini.
Aidha alisema Benki ya Stanbic katika kipindi hiki, imeendelea kukua kwa kasi na sasa ni benki namba tatu nchini kutokana na ripoti ya hesabu za mwaka 2024.
“Katika kipindi hiki chote tumekua mshirika wa kuwaletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii wateja na jamii zinazotuzunguka, na kubwa zaidi tunajivunia ushiriki wetu katika kuchangia ufanikishaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ya taifa letu katika sekta mbalimbali za uchumi,” amesema Max.
Kasi ya ukuaji wa benki ya Stanbic imeendelea kukua ikihudumia watanzania kupitia matawi 11, na mengine sita yakiwa mbioni kufunguliwa mwaka huu huku moja kati ya hayo likiwa mkoani Geita.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita Martin Shigela alihitimisha kwa kuipongeza benjki hiyo akisema kuwa imekuwa mstari wa mbele katika kujishughulisha na shughuli za wanawake mkoani humo.


