Kongole Tanzania kudhibiti kifua kikuu, vita iendelee

VITA dhidi ya magonjwa ilianza tangu nchi ilipopata uhuru wakati Mwalimu Julius Nyerere alipotangaza maadui watatu wa Tanzania kuwa ni ujinga, maradhi na umasikini.

Tangu hapo awamu zote za serikali zimepambana kutokomeza maadui hao na bado juhudi zinaendelea na mafanikio yanaonekana kwani inaelezwa hivi sasa Tanzania imepiga hatua kubwa kupunguza maambukizi mapya ya Kifua Kikuu (TB).

Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani 2025, Machi 24 jijini Arusha alisema maambukizi ya TB yamepungua kutoka wagonjwa 306 kwa kila watu 100,000 mwaka 2015 hadi wagonjwa 183 kwa kila watu 100,000 kwa mwaka 2023, ikiwa ni sawa na punguzo la asilimia 40.

Alisema kiwango hicho kimefanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 13 duniani zilizo katika hatua sahihi kufikia lengo la dunia la kupunguza maambukizi mapya kwa asilimia 50 na vifo kwa asilimia 75 ifikapo 2025, hivyo kuwa katika njia sahihi ya kutokomeza ugonjwa huo ifikapo 2030.

Kwa mujibu wa Dk Mollel, vifo hivyo vitokanavyo na ugonjwa huo, vimepungua kutoka 56,000 mwaka 2015 hadi vifo 18,400 mwaka 2023, ikiwa ni sawa na punguzo la asilimia 68.

Tunawiwa kuipongeza serikali kwa hatua hii kwani ni utekelezaji wa eneo moja la ndoto za Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere na viongozi wengine waliomfuatia, akiwemo kiongozi wa sasa Rais Samia Suluhu Hassan.

Tunaamini hatua hizi zimechangiwa na jitihada kubwa zilizochukuliwa na serikali kuboresha huduma za kifua kikuu nchini, ikiwemo kuongeza wigo wa mtandao wa huduma za uchunguzi na upimaji wa ugonjwa huo na ushirikishwaji wa jamii kupitia kampeni mbalimbali.

Kampeni hizo ni pamoja na kuhamasisha jamii na wadau kuhusu wajibu wao katika kuchochea jitihada za kutokomeza ugonjwa huo nchini na hili tunashauri liendelee kwa kasi zaidi ili kutokomeza kabisa ugonjwa huo na mingine kabla hata ya 2030.

Tunashauri nguvu zaidi iwekwe katika elimu kwa jamii kuhusu dalili za ugonjwa huo ili wenye dalili wasichelewe kuchukua hatua mapema na hivyo kudhibiti mnyororo wa maambukizi mapya katika jamii.

Tunafahamu ipo kampeni inayoendelea sasa katika halmashauri 76 katika mikoa tisa ili kuibua wagonjwa na kuwaanzishia tiba iliyoanzishwa na wizara kwa kuhirikiana na wadau kuanzia Desemba 2024 hadi Machi 2025 na tunashauri kasi iendelee.

Kupitia kampeni hiyo tayari wagonjwa 9,585 wa Kifua Kikuu wameibuliwa na kuwekwa kwenye matibabu sawa na asilimia 66 ya lengo la kuibua wagonjwa 14,471.

Hatua hizi ndizo zimetusukuma kuiponeza serikali na kushauri vita hii iendelee kuzuia madhara yanayochangiwa na wananchi kuugua kifua kikuu, ikiwemo kupoteza nguvu kazi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button