Kuagiza bahari ifukiwe kupata ardhi

ZANZIBAR : CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kitaielekeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ianze mpango wa kufukia bahari ili kupata ardhi kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2025-2030 imeeleza ardhi ni rasilimali muhimu inayotumika kwa ajili ya shughuli za maendeleo kikiwamo kilimo, viwanda, utunzaji wa mazingira na uwekezaji.
“CCM itaendelea kuzisimamia sera na sheria zitakazohakikisha matumizi endelevu ya ardhi ili kuleta maendeleo kwa wananchi,” imeeleza Ilani. CCM imeeleza katika kipindi cha 2025 – 2030, SMZ ianzishe na kuimarisha mifumo ya dijiti ya usajili wa ardhi. Pia, chama hicho kinataka SMZ iendelee kufanya mapitio ya sera, mipango na sheria za ardhi ili kuendana na mabadiliko ya kijamii, kiuchumi na kimazingira na utekelezaji wa mkakati wa usimamizi wa ardhi.
Ilani inaeleza SMZ itaagizwa ipime na kuyatangaza maeneo ya kudumu ya ardhi kwa matumizi ya kilimo, matumizi ya viwanda na uwekezaji, maeneo ya ardhi yaliyo wazi, maeneo yaliyotengwa kwa matumizi maalumu, maeneo ya burudani na maeneo kwa matumizi ya jamii. SOMA: SMZ yapongezwa uwekezaji sekta ya afya
CCM inataka SMZ iendelee kutambua na kusajili ardhi katika maeneo ya Unguja na Pemba na iweke mpango wa upangaji na upimaji wa visiwa vidogo kulingana na matumizi ya wananchi na uwekezaji wa visiwa hivyo. Ilani inaeleza kwamba chama hicho kinataka SMZ iendelee kupima na kuyapangia matumizi maeneo yote ya ardhi ya akiba ili kuongeza thamani ya maeneo hayo.



