Kuendeshwa na Mafanikio: Safari isiyo ya kawaida ya Laurence Mollel

WANASEMA, “Bahati ya mwenzio usiilalie mlango wazi,” lakini katika biashara, bahati huja kwa wale wanaothubutu kufanya maamuzi sahihi na kuwekeza juhudi zao kikamilifu.
Hilo ndilo lililotokea kwa Laurence Mollel, dereva wa teksi jijini Arusha, ambaye zamani alikuwa mfanyakazi wa kawaida katika kampuni ya bima.
Mwaka 2021, Mollel aliamua kuacha kazi yake ya ofisini licha ya kutokuwa na mpango madhubuti wa baadaye. Alijua moja tu: kazi ya kukaa nyuma ya dawati haikumletea mafanikio aliyotamani.
“Kazi ilikuwa ya kurudia rudia, muda ulikuwa mgumu, na mshahara haukuwa ukitosha kukidhi mahitaji yangu,” anakumbuka.

Kwa ujasiri mkubwa, alinunua gari lililotumika na kujiunga na huduma ya Indrive kama dereva wa ride-hailing.
“Nilitaka uhuru wa kudhibiti muda wangu na kipato changu. Ride-hailing ilinipa nafasi hiyo,” anasema kwa tabasamu.
Haikuchukua muda mrefu — mwaka mmoja baadaye, maisha yake yalibadilika kabisa. Aliweza kununua gari la pili na kulikodisha kwa dereva mwingine, akiongeza kipato zaidi.
Hata hivyo, hakuishia hapo. Alipoona magari ya watalii kama Land Cruiser yakikatiza barabara za Arusha, ndoto yake ilipanuka zaidi. Aliweka akiba kidogo kidogo na kufanikisha kununua Toyota Alphard, gari linalomuwezesha kutoa huduma za hadhi zaidi kwa wateja wa uwanja wa ndege na watalii.
Kuanzishwa kwa Bolt katika soko la Arusha kulimfungulia fursa zaidi kupitia majukwaa mawili tofauti. Kile kilichoanza kama jaribio sasa ni biashara halisi, yenye mwelekeo na malengo makubwa.
Kwa mujibu wa tovuti ya Paylab.com, madereva wa teksi nchini Tanzania hupata kati ya TSh651,000 hadi TSh1.5 milioni kwa mwezi, huku makarani wa ofisini wakipokea wastani wa TSh765,000. Takwimu hizi zinaonesha wazi kuwa sekta ya ride-hailing inalipa zaidi pale inapoendeshwa kwa bidii na weledi.
Mollel anakumbuka mshahara wake wa mwisho alipokuwa kazini kwenye bima na sasa anatabasamu anapoangalia alipoifikisha safari yake.
“Sekta hii imenibadilishia maisha,” anasema huku akirekebisha kioo cha nyuma cha gari lake. “Sasa sifanyi kazi tu najenga maisha yangu.”



