Usile matunda mchanganyiko zaidi ya mawili– Mtaalamu

DAR-ES-SALAAM : MTAALAMU wa lishe kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Husna Faraji, ameeleza kuwa ulaji wa matunda mchanganyiko zaidi ya aina mbili kwa mlo mmoja unaweza kuongeza uzito kupita kiasi na kuongeza hatari ya kupata magonjwa ya moyo na shinikizo la damu.

Akizungumza na Daily News Digital, Husna alisema kiafya mtu anashauriwa kula tunda moja au mawili kwa mlo mmoja ili kuepuka kuingiza kiwango kikubwa cha sukari mwilini. “Kwa maeneo ya mjini, hatupendekezi kula matunda zaidi ya aina mbili kwa wakati mmoja. Shughuli nyingi za sasa hazihusishi mwendo, hivyo ulaji wa matunda mengi unachangia kuongezeka kwa sukari na hatimaye uzito mkubwa,” alisema.

Ameeleza kuwa matunda ya aina mbili yanaweza kutumika kwa vipindi tofauti vya siku, kwa mfano ndizi na parachichi asubuhi, chungwa na tango mchana, na zabibu jioni.SOMA: Bukoba Vijijini wapanda miti 500 ya matunda

Husna alionya dhidi ya tabia ya kuchukua juisi badala ya kula matunda yenyewe, akisema usagaji wa matunda hupunguza nyuzinyuzi muhimu na virutubisho, huku ukisababisha ulaji wa sukari nyingi kwa wakati mmoja. “Juisi haina nyuzinyuzi zinazosaidia mmeng’enyo wa chakula, na kutumia matunda mengi kwa wakati mmoja kunakuweka kwenye hatari ya magonjwa yasiyoambukiza,” alisisitiza.

Akizungumzia muda wa kula, Husna alishauri vyakula vya jioni viandaliwe mapema, kupunguza ulaji wa wanga na sukari usiku, na kuongeza mboga za majani. “Ukila chakula kingi jioni mwili unakosa muda wa kukichoma kwa sababu mmeng’enyo hupungua ukiwa umelala, hivyo kuongeza hatari ya uzito kupita kiasi,” alisema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button