Kulipa kodi ni uzalendo, kila mmoja awajibike

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) juzi ilitangaza kuvunja rekodi ya makusanyo kwa mwaka 2024 baada ya kukusanya Sh trilioni 16.528 kuanzia Julai hadi Desemba kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/2025.

Kwa mujibu wa takwimu, kwa Desemba 2024 pekee mamlaka hiyo imevunja rekodi ya kukusanya mapato ya Sh trilioni 3.587, kiwango cha juu kabisa kukusanywa kwa mwezi mmoja tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo mwaka
1995.

Katika taarifa yake kwa wanahabari juzi, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, ametaja sababu takribani nane zilizowezesha makusanyo hayo, ikiwamo kusimamia ulipaji kodi wa hiari kwa walipakodi pamoja na kusikiliza na kutatua changamoto zao.

Sababu nyingine ni kusimamia ushirikiano baina ya TRA, wizara, taasisi na ofisi nyingine za serikali kusimamia sera za kodi na ufanyaji wa biashara nchini, kuongezeka kwa utendaji kazi mzuri, nidhamu na ubunifu kwa watumishi
wa TRA.

Ipo pia, sababu ya kuendelea kuboresha mahusiano na wafanyabiashara kwa kutenga siku ya Alhamisi ya kila wiki kuwa siku maalumu ya kusikiliza walipakodi kupitia ofisi zote za TRA, na Desemba ni mwezi wa kutoa shukrani kwa walipakodi wote.

Kwa makusanyo haya ya kodi, TRA wanastahili pongezi kwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Lakini pia, makusanyo haya yanaonesha wapo Watanzania wanaoona umuhimu kulipa kodi ili zifanye kazi ya kuwaletea maendeleo. Hawa nao wanastahili pongezi nyingi.

Wakati tukipongeza ufanisi huu katika kodi, ni muhimu kueleza kwamba bado makusanyo haya yanaweza kuongezeka maradufu kwa sababu takwimu zinaonesha bado wanaolipa kodi nchini ni wachache ikilinganishwa na idadi ya watu.

Kwa hiyo bado ipo kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha idadi inaongezeka tena walipe kwa hiari kama ambavyo serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikisisitiza.

Hakuna asiyefahamu umuhimu wa kodi hivyo hakuna sababu ya watu ama kutolipa kodi kabisa au kukwepa kodi.
Hawa ni wahujumu wa uchumi, na si wazalendo, kwa hiyo wanastahili kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Tunafarijika kuona TRA imeendelea kuchukua hatua kuhakikisha Watanzania wengi wanapata uelewa na elimu kuhusu kodi, ikiwamo kuwashirikisha viongozi wa dini nchini.

Hili ni kundi muhimu katika jamii, kwa hiyo kama likielimishwa na kupata elimu hii muhimu, litakuwa na mchango
mkubwa kuongeza makusanyo ya kodi, hasa ikizingatiwa taasisi zao zimekuwa ni wachangiaji wazuri wa kodi nchini.

Tunaamini elimu watakayopata na kwenda kuwaelimisha waumini wao itakuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi eneo la kodi hasa wakati huo ambao, Rais Samia ameunda Tume ya Maboresho ya Kodi ili kuangalia mfumo wa kodi na kushauri kuhusu eneo hilo.

Habari Zifananazo

Back to top button