KUWASA yazindua mfumo kudhibiti upotevu wa maji

KIGOMA; Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kigoma (KUWASA), kwa kushirikiana na Kampuni ya CollectTech Limited, imezindua mfumo mpya wa kiteknolojia uitwao Amanzi App unaolenga kuwezesha wananchi kutoa taarifa za mivujo ya maji moja kwa moja kwa mafundi kupitia simu za mkononi.
Mkurugenzi Mtendaji wa KUWASA, Poas Kilangi, akitoa taarifa wakati wa uzinduzi wa mfumo huo alisema kuwa mpango huo unakuja ukiwa ni kuzuia hasara ya maji yanazozalishwa kupotea baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji wenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 42 kwa siku, hivyo maji mengi kuzalishwa lakini pia miund mbinu chakavu imesababisha maji yanayozalishwa kupotea.
Kilangi alisema kuwa KUWASA imekuwa ikikabiliwa na upotevu wa maji kwa kiasi cha asilimia 41 ya uzalishaji wake hali inayosababisha hasara ya kiasi cha shilingi bilioni 2 kwa mwaka.
Hivyo, kuanzishwa kwa App ya Amanzi ni hatua ya kimkakati katika kudhibiti changamoto hiyo wakati mamlaka ikiendelea pia na ubadilishaji wa miundo mbinu chakavu kuweka miundo mbinu mipya ambayo itathibiti upotevu huo wa maji.

Akizungumza katika uzinduzi huo Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye, alisema kuwa uzinduzi wa Amanzi App ni hatua kubwa katika kuboresha huduma za maji na kuhakikisha rasilimali hiyo muhimu haipotei ambapo ametumia nafasi hiyo kuwahimiza wakazi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji na Mamlaka nyingine za maji mkoani humo kutumia teknolojia hiyo kama suluhisho la tatizo la upotevu wa maji unaosababishwa na mivujo.
Pia ametoa wito kwa waendesha pikipiki za abiria (bodaboda) kutumia nafasi yao ya kufika maeneo mbalimbali kuchangia katika kukusanya taarifa za mivujo kwa kutumia App hiyo, hivyo kusaidia serikali kuokoa fedha zinazotumika katika uzalishaji wa maji.
Uzinduzi wa mfumo huo ulishuhudiwa na waendesha pikipiki za abiria (bodaboda) zaidi ya 200 kutoka Manispaa ya Kigoma Ujiji ambao wamechukuliwa kama wadau muhimu katika kusaidia kufanikisha lengo la upatikanaji wa taarifa za mivujo kwa haraka kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kigoma.



