LAAC yaibana Halmashauri Mji wa Nanyamba

KAMATI ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeutaka Uongozi wa Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara kuhakikisha inatumia fedha za serikali kwa malengo yaliyokusudiwa kwa kutekeleza miradi ya maendeleo na sio vinginevyo.

Hayo yamesemwa jana na mwenyekiti wa kamati hiyo, Halima Mdee baada ya Kamati hiyo kufanya ziara ya ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa hospitali ya halmashauri hiyo utaogharimu zaidi ya Sh bilioni 3 hadi kukamilika.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi huo, Mdee ameusisitiza uongozi huo kwamba serikali inapoleta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo hospitali hiyo zitumike kama inavyotarajiwa ili kuwatendea haki wananchi wa maeneo husika na kurahisisha huduma.

Kukamilika kwa mradi huo kutarahisisha upatikanaii wa huduma mbimbali za afya kwa Wananchi wa maeneo hayo hasa zile ambazo awali zilikuwa hazipatikani kwa Wananchi wa maeneo hayo kama vile upasuaji, mionzi Ex-ray na zingine.

Mganga mfawidhi wa hospiltali hiyo ya Mji Nanyamba Selemani Kasuguru amesema mpaka sasa huduma ambazo zinatolewa hospitalini hapo ikiwemo huduma ya uzazi kwa wajawazito, upasuaji kwa akina Mama wajawazito, wagonjwa wa nje (OPD), kulaza wangonjwa, maabara na zingine.

‘’Faida ya mradi huu kwa kiasi kikubwa umesogeza huduma kwa Wananchi kutokana hivi sasa wanapata huduma hii kwa karibu ’,amesema Kasuguru

Baadhi ya Wananchi wa maeneo hayo akiwemo Mariamu Hamisi ameipongeza Serikali kwa kuwaletea mradi huo kwenye eneo lao kwani utawaondolea changamoto ambazo walikuwa wakikumbana nazo siku za nyuma kabla ya ujenzi huo kama vile huduma za upasuaji kwa akina Mama wajawazito hasa wakati wa kujifungua.

“Sisi akina Mama tunapokabiliwa na suala la uzauzito kwakweli tunahitaji tuwe na huduma kama hii kwa karibu kwasababu kuna matatizo ambayo mjamzito anaweza kupata wakati wa kujifungua akahitaji msaada wa haraka mfano upasuaji kwahiyo ilikuwa inatulazimu kutoka nje ya hapa ila sasa hivi tunazipata hapa hapa”,amesema Hamisi

Ujenzi huo ilianza mwaka 2018 na mpaka sasa upo kwenye hatua ya umaliziaji.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x