Laigwanani walaani waandishi kupigwa Ngorongoro

VIONGOZI wa Kimila wa Jamii ya Kimasai maarufu Laigwanani wamelaani kitendo kilichofanywa na wakazi wa jamii hiyo cha kuwapiga na kuwashambulia waandishi wa habari waliokuwa katika shughuli za utekelezaji wa majukumu ya kazi katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) mkoani Arusha.

Malaigwanani walisema hayo jana katika kijiji cha Nayobi kata ya Kapenjiro wilayani Ngorongoro na kusema kuwa waliofanya tukio hilo wanapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria bila kuonewa haya kwani wanawachonganisha Wamasai walio tayari kuhama kwa hiari yao na serikali  ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Mmoja wa Laigwanani wa kimasai mkazi wa Nayobi Ngorongoro aliyejitambulisha kwa jina la Ikoyo Roinge alisema hayo wakati wakizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa mila ya upatanisho ,kulaani na kukemeaa kitendo hicho cha kupigwa kwa waandishi na kusema kitendo hicho hakitarudiwa tena.

‘’Tunalaani kitendo kilichotokea Agosti 15 mwaka huu cha waandishi wa habari kupigwa wakiwa na mkalimani wao na tunalaani sana jambo hilo lisitokee tena kwa sababu wamepigwa na kujeruhiwa waandishi hao bila hatia yoyote,”

‘’Ndio maana leo tunafanya zoezi la upatanisho kwa wazee wote, wamama, viongozi wa mila na jamii kwa ujumla kwa kuwa uhamisho ni jambo la hiari na sio vinginevyo.’’ alisema Roinge.

Kiongozi wa Kikatoliki Parokia ya Nainokanoka ,Katekista Edward Leyani alisema wanawaombea msamaha wale wote waliohusika na tukio hilo kwa kuwa Mungu ndio mpatanishi wa kila jambo na huwa hapendi uvunjifu wa amani katika eneo lolote kwani wote ni watu wake.

Leyani alisema wale wote waliokuwa tayari walifanya maamuzi yao kwa hiari yao na wale wote wanaodai kuwa kuna watu wanawalazimisha wananchi wa Ngorongoro kuhama hiyo sio kweli kwani wanafanya hivyo kwa maslahi yao.

Alisema na kusisitiza kuwa wananchi wa jamii ya kimasai wako tayari kuhama kwa kutii maagizo ya serikali inayoongozwa na Rais Samia na kusema kuwa hawatakubali kurubuniwa na mtu,kikundi kwa maslahi yao kwani maamuzi ya kuhama ni yao wenyewe na sio kulazimishwa.

Laigwanani Ndwala Ndoishie akisoma tamko la jamii ya kifugaji ya Kimasai alisema wamefanya mila kwa kuchinja Ng’ombe watatu, Ng’ombe mmoja kwa kumwaga damu ya kuomba radhi kwa uongozi wa NCAA, Ng’ombe wa pili kuomba radhi kwa serikali na Ng’ombe wa tatu kuomba radhi kwa Rais kufuatia tukio hilo.

‘’Kwa umoja wetu wamasai na wananchi wote tuishio ndani ya hifadhi ya  Ngorongoro, tunatoa tamko la utii kwa mama juu ya nia njema  yake ya kututaka  kuhama kwa hiyari kwamba tumepokea neno hilo kwa moyo mmoja na kwa Pamoja tunasema tuko tayari kuhama.’’ alisema Laigwanani Ndoishie.

 

Aidha Laigwanani huyo katika tamko lake alisema kuwa serikali iwachukulie hatua kali za kisheria  wale wote wanaopotosha na kujaribu kukwamisha  zoezi hilo kwa maslahi yao binafsi  na kuchonganisha na serikali yenye dhamira njema kwa  wamasai wa Ngorongoro.

‘’ Rais sisi Wamasai tunawafahamu wapotoshaji hao wakiwemo  wanasiasa, wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi, wanaharakati,  asasi za kiraia na jumuiya za nje ambao wamekuwa wakitumia pesa nyingi kutulaghai na kutufanya mitaji yao hali inayopelekea  kutufanya tuendelee kuwa masikini zaidi wakati wao na familia zao wanaishi nje ya hifadhi ya Ngorongoro na sisi kutufanya tuendelee kuwa watumwa wao na sasa tunasema imetosha.’’ ilisema sehemu ya tamko hilo.

Habari Zifananazo

Back to top button