Lissu ‘awachana’ viongozi upinzani kung’ang’ania madaraka

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu amesema viongozi wa vyama vya upinzani pekee wameng’ang’ania madaraka kwa kupinga ukomo wa madaraka hayo.

Pia, ameitaka Kamati Kuu ya chama hicho kuhakikisha katika mkutano mkuu wa uchaguzi wa nafasi ya mwenyekiti wawepo viongozi wa dini pamoja na mabalozi kama watazamaji, wakishuhudia utaratibu wote kuanzia upigaji kura, kuhesabu kura na kutangaza mshindi.

Lissu alisema hayo jana wakati akitoa salamu za mwaka mpya na kuongeza: “Kwa uzoefu wetu kama nchi tangu tuingie kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa ni viongozi wa upinzani tu ndio wameng’ang’ania madarakani kwenye vyama vyao kwa muda mrefu zaidi, hatuhitaji kuthibitisha ukweli huu kwa kuwataja majina”.

Aliongeza, “Kama lengo la ukomo wa madaraka ni kudhibiti ving’ang’anizi wa madaraka na kuhakikisha utaratibu wa kuachiana madaraka kwa njia za kikatiba, ukomo wa madaraka unawahusu viongozi wote wa kisiasa bila kujali wanajitolea au wanalipwa mishahara”.

Pia, alisema jambo hili linarudisha nyuma harakati za chama hicho za kudai mfumo bora wa uchaguzi.

“Hili ni mojawapo ya doa kubwa katika harakati za kudai mfumo bora wa uchaguzi, sisi sote ni mashahidi kwa namna CCM (Chama Cha Mapinduzi) imetukejeli mara nyingi kwa hoja kwamba vyama vyetu ni mali binafsi za vyama vyetu na familia zao sababu ya kukaa madarakani kwa muda mrefu,” alisema.

Akizungumzia uchaguzi wa mwenyekiti wa chama hicho, Lissu amependekeza ushiriki wa viongozi wa madhehebu ya dini kama watazamaji katika uchaguzi huo ili uwe huru na haki.

“Napendekeza kuwa pamoja na wazee wastaafu wa chama watakaopatikana kusimamia uchaguzi, kamati kuu iwaombe viongozi wa madhehebu ya dini kuhudhuria mkutano mkuu kama wageni waalikwa na watazamaji ili kuzuia mipango ya waovu kuvuruga uchaguzi wetu, kamati kuu pia iwaite wawakilishi wa balozi wa nchi rafiki washiriki kama watazamaji wa uchaguzi wetu,” alisema.

Aidha, Lissu ameitaka kamati ya wazee wastaafu wa chama itakayoteuliwa na kamati kuu kusimamia uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki.

“Napendekeza kuhakikisha hatua zote za uchaguzi, ikiwa ni pamoja na kupiga na kuhesabu kura na kutangaza matokeo zinafanyika wakati wa saa za mchana na kwa vyovyote vile zisifanyike wakati wa usiku au wa giza,” alisema.

Aliongeza, “Kuhakikisha kwamba shughuli za upigaji kura, kuhesabu kura na kutangaza matokeo ya uchaguzi zinafanyika kwa uwazi mbele ya wajumbe wa mkutano kuondoa uwezekano wa kuingiza kura haramu au kubadilisha matokeo”.

Habari Zifananazo

Back to top button