Maagizo ya Waziri Mkuu ukamilishaji miundombinu mwendokasi yazingatiwe

TANZANIA inapiga hatua kubwa katika ujenzi wa miundombonu ya usafirishaji katika Afrika Mashariki na Kati.

Miongoni mwa mafanikio katika sekta hiyo ya usafirishaji na kuigwa na nchi nyingine ni ujenzi wa miundombinu ya mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) maarufu mwendokasi unaotekelezwa Dar es Salaam.

Ujenzi wa miundombinu hiyo katika barabara kuu umewekwa katika awamu nne ambapo awamu ya kwanza inatumika na awamu nyingine tatu zinaendelea kujengwa zikiwa katika hatua mbalimbali.

Awamu ya kwanza ya mradi inatoka Kimara hadi Kivukoni, Awamu ya Pili ni ya Mbagala hadi Gerezani, Awamu ya Tatu inatoka Gongo la Mboto hadi Gerezani na Awamu ya Nne inatoka Tegeta hadi Morocco.

Kutokana na hilo, serikali kupitia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa juzi ilitoa maagizo kwa waendeshaji wa mradi huo wafanye kazi usiku na mchana kukamilisha maeneo yaliyobaki ili kuwezesha safari za katikati ya jiji kufanyika ikijumuisha za Mbagala zinazotarajiwa kuanza mwezi huu.

Waziri Mkuu aliagiza hayo alipokagua mabasi mapya kwa ajili ya awamu ya pili ya mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT-2) na miundombinu, ikiwemo kituo kikuu cha mabasi ya awamu hiyo cha Mbagala Rangi Tatu wilayani Temeke na kituo cha Gerezani wilayani Ilala.

Pamoja na ukaguzi huo, pia Majaliwa alitembelea ujenzi wa kituo cha kujazia gesi kwa ajili ya mabasi hayo, kinachojengwa katika kituo cha Mbagala Rangi Tatu.

Tunamatumaini kwamba maagizo haya ya Waziri Mkuu yatatekelezwa ipasavyo kwa wahusika kufanya kazi usiku na mchana kama alivyoagiza kwa kuwa katika ziara yake hiyo aliambatana na viongozi wa taasisi na mamlaka zinazosimamia mradi huo wakiwemo mawaziri na makatibu wakuu.

Mradi wa BRT-2 unaotarajiwa kuanza mwezi huu, unatarajiwa kuongeza ufanisi wa usafiri wa umma Dar es Salaam na kutoa huduma ya kisasa, salama na ya haraka kwa wananchi na kuondoa changamoto ya usafiri wanayokumbana nayo wakazi wa jiji hilo.

Hivi karibuni Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) ulisaini mikataba na watoa huduma binafsi wanne wakiwemo watatu wa Kitanzania kwa ajili ya kuleta mabasi mapya 932 kwa awamu ya kwanza na ya pili hadi ifikapo Oktoba mwaka huu.

Hatua hii ni kubwa na inahitaji kasi kubwa vilevile ya ukamilishaji miundombinu unaoendelea ili kutokwamisha hatua yoyote hasa ikizingatiwa Dar es Salaam ni mji wa biashara.

Wananchi na wakazi wa Dar es Salaam na wageni wanaoingia na kutoka wanategemea kwa kiasi kikubwa mradi huu uwasaidie kuondoa kero ya usafiri na si kuwaongezea kero, hivyo tunaunga mkono maagizo kwa wahusika kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana kukamilisha hilo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button