Maambukizi ya VVU Mama kwa Mtoto yapungua

Usalama wa watoto wanaozaliwa kutopata maambukizi ya VVU hivi sasa ni mkubwa kutokana na jitihada za Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo
Waziri wa Afya Jenista Mhagama amezindua ripoti ya utafiti wa viashiria na matokeo ya UKIMWI mwaka 2022 - 2023, Songea mkoani Ruvuma leo Novemba 29, 2024.

RUVUMA – Waziri wa Afya Jenista Mhagama amesema kiwango cha maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yamepungua kutoka asilimia 18 mwaka 2010 hadi asilimia 8.1 mwaka 2023.

Waziri Mhagama amesema hayo Novemba 29,  wakati wa ufunguzi wa kongamano la kitaifa la kisayansi la masuala ya UKIMWI pamoja uzinduzi na usambazaji wa ripoti ya utafiti wa viashiria na matokeo ya UKIMWI mwaka 2022 – 2023 uliofanyika Songea mkoani Ruvuma.

Waziri Mhagama amesema usalama wa watoto wanaozaliwa kutopata maambukizi ya VVU hivi sasa ni mkubwa kutokana na jitihada za Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kuwekeza na kutekeleza afua mbalimbali za masuala ya VVU na UKIMWI.

Advertisement

Image

“Nishukuru sana kwa juhudi za wadau wote ambao wanajielekeza katika kuhakikisha maisha yanaendelea kwa WAVIU na watoto wanaozaliwa katika mahusiano mbalimbali hapa nchini wanakua salama,” amesema Waziri Mhagama.

Aidha, Waziri Mhagama ameishukuru Tume ya Taifa Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) kwa kuendelea kuratibu suala zima la mapambano ya VVU na UKIMWI kwa kutengeneza mikakati unganishi na shirikishi ambayo itasaidia katika kufikia mafanikio na mikakati iliyowekwa.

Waziri Mhagama ametoa wito kwa kila mmoja kushiriki katika kulinda na kuthamini mafanikio yaliyofikiwa ikiwa ni pamoja na kuondoa unyanyapaa kwa watu wanaishi na maambukizi ya VVU.

SOMA: Watu zaidi ya laki moja wagundulika na VVU 2023

Naye Mkuu wa Wilaya ya Songea Kapenjama Ndile ambaye amemuwakilisha Mkuu wa Mkoa huo amesema Mkoa huo umepata mafanikio ya kupambana na maambukizi mapya ya VVU kutoka asilimia 5.6 mwaka 2017 hadi 4.9 mwaka 2022 ikiwa sawa na asilimia 0.7 huku viwango vya kitaifa ikiwa na asilimia 2.8.

Wiki ya maadhimisho ya kitaifa ya siku ya UKIMWI duniani yanaendelea mkoani Ruvuma ambapo yanatarajiwa kufikia kilele Desemba 1 ambapo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Philip Mpango akitarajiwa kuwa mgeni rasmi