Mabadiliko tabianchi, mgogoro mpya wa afya wa kuangaliwa

“HAKUNA swali mabadiliko ya tabianchi ni mgogoro wa afya pia, ongezeko la joto, vimbunga, mafuriko, usalama mdogo wa chakula, ongezeko la magonjwa ya mfumo wa hewa na kuongeza kasi ya maambukizi ya magonjwa yanagharimu ustawi wa afya ya jamii na mifumo ya afya ulimwenguni kote,” anasema Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Ghebreyesus.

Tedros kupitia video iliyopo katika mtando wa X, anasema ni muhimu kufanikisha malengo ya Mkataba wa Paris (COP) ya kupunguza ongezeko la joto lisifikie 1.5 ili kulinda afya ya jamii.

Anasema WHO inaungana na ripoti zilizotolewa na wadau wa mabadiliko ya tabianchi kupunguza uharibifu wa anga na kuongeza usawa wa afya.

“Ninatazamia COP28 ambayo kwa mara ya kwanza itajumuisha wadau wa afya kwa pamoja lazima tuendelee kukumbusha dunia kwamba athari za hali ya hewa ni athari za afya,” alisisitiza.

Anatoa wito kwa viongozi wote wa dunia wanaoshiriki COP28 kujikita katika kulinda afya ya watu wote.

Katika ripoti ya awali ya WHO mabadiliko ya hali ya hewa, yanaweza kuwa na madhara makubwa kwa viashiria muhimu vya afya kama vile athari kwa usalama wa chakula, ubora wa hewa na maji, mifumo ikolojia na usalama wa miundombinu ya afya.

Matukio ya magonjwa yanayoenezwa na wadudu na magonjwa yanayoenezwa na maji, kipindupindu, kukabiliwa na moshi na moto wa nyikani, mafuriko na athari za kiafya na lishe zinazohusiana na ukame, huongeza utapiamlo.

Ongezeko la milipuko ya magonjwa yanayoenezwa na mbu kama malaria katika maeneo ya nyanda za juu kwenye kawaida ya kuwa baridi, hatari ya homa ya Bonde la Ufa, idadi kubwa ya watu walioathiriwa na magonjwa ya kuambukiza kama surua na uti wa mgongo.

Pia kukatizwa kwa huduma za afya kutokana na ukosefu wa maji au uharibifu wa miundombinu ya afya kutokana na mafuriko na vimbunga ni chanzo kuvuruga afya ya jamii.

Athari kwa nchi

Katika mahojiano na HabariLEO, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu anakiri mabadiliko ya tabianchi yamedhihirika na anasababisha athari katika sekta ya afya kama sekta zingine.

Ummy anasema kubwa wanaloliona ni milipuko ya ugonjwa wa kipindupindu.

“Japo Tanzania bado hatujapata moja kwa moja lakini Msumbiji kutokana na kimbunga na mafuriko vimesababisha ongezeko la magonjwa ya milipuko.

Anasema kwa upande wa Tanzania wanaangalia upande wa malaria ambapo zamani kuna maeneo walikuwa wanajua hayana malaria lakini kutokana na mabadiliko ya tabianchi sasa maeneo hayo kuna malaria.

Ummy anabainisha pia uhusiano mwingine unapatikana katika magonjwa yasiyoambukiza kupitia nishati chafu inayoathiri mfumo wa upumuaji na ongezeko la joto.

“Sisi tunaongozwa na miongozo ya WHO ambayo sasa inakamilisha mikakati ambayo itazinduliwa hivi karibuni jinsi gani mabadiliko ya tabianchi yanavyoathiri afya, kwa hiyo tunasubiri mwongozo wao uje na tunaamini utatusaidia tukawa na mikakati mahususi ya kuitikia,” anasema Ummy.

Nini kinatokea kiafya

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya ndani wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Elisha Osati, anasema mabadiliko ya tabianchi yanaweza kuwa na joto, baridi kali, mvua nyingi na ukame.

Dk Osati anasema joto likiwa kali inasababisha watu kupoteza maji mengi mwilini na damu inakuwa nzito kutokana na kupoteza maji. Anasema mtu anabaki na chumvichumvi na hivyo hali hiyo inaweza kuathiri figo, kupata shida kwenye ubongo kwa kupata kiharusi na mapigo ya moyo kwenda haraka.

“Kwenye ubongo sehemu inayochuja joto inaathirika kila joto linavyoongezeka na mwili utashindwa kufanya kazi kwani unafanya kazi kwenye joto la 36 hadi 38, haitakiwi kuvuka mfano mazingira yanakuwa na joto ya chini kuliko mwili na kama mazingira yana joto jingi mwili unashindwa kupoteza joto.

Anasema athari kwa watoto wadogo na wazee ni kubwa kwani miili yao imepungua mafuta ambayo yanasaidia kuongeza joto.

“Baridi pia ikiwa nyingi mwili unashindwa kufanya kazi zake na hapo inaweza fikia mtu akapoteza maisha kwa kupata tatizo linaloitwa Haipothemia baada ya joto kuwa la chini sana, moyo kuathirika,” anaeleza Dk Osati.

Madhara mengine anasema wakati wa mafuriko miti huanguka, mawe yanadondoka milimani, upepo mkali, mvua kubwa inaleta mafuriko na taka zinapozagaa, magonjwa ya kuhara, kipindupindu yanakuwepo na maji yanayotuama husababisha wadudu kuzaliana hivyo malaria inaongezeka.

“Kuna magonjwa yanayotokana na uharibifu wa mazingira, vumbi nyingi inaathiri mapafu na njia ya hewa kwa maeneo ya vijijini kina mama wanalazimika kutumia mavi ya ng’ombe kama kuni, moshi unawaathiri mapafu wakati wa kupika na vumbi inaweza kuleta shida ya kukohoa na mapafu kushindwa kufanya kazi.

Pia anasema afya ya akili inaweza kuathirika kutokana na kupoteza maji inaathiri ubongo na kupoteza umakini ambapo hiyo hali inaleta msongo wa mawazo na baadaye sonona na kama mtu alikuwa na hatari inaongezeka zaidi.

Meneja wa Maabara Kuu ya Taifa, Ambele Mwafulango anasema kunapokuwa na joto kali kuna wadudu ambao wanakaa kwenye vumbi katika mabadiliko hayo wanabadilika kutoka hali ya mwanzo kuja nyingine ambapo mvua ikinyesha wanatoka kuingia kwa wanyama na kusababisha homa ya bonde la ufa.

“Si tu vinyesi hata utupaji wa taka unahamisha wadudu kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa mafuriko na mabadiliko ya hali ya hewa yanapotokea lazima hatua zichukuliwe,” anasisitiza.

Mambo ya kuzingatia  

Dk Osati anasema endapo mtu ataathiriwa na joto ni vizuri akapelekwa hospitali endapo mabadiliko yataonekana na kama atahitaji kuongezewa maji ataongezewa kwa ajili ya kupooza mwili.

Anasema kama ni baridi anapaswa kula vyakula vya moto na kujifunika mavazi yenye kuleta joto.

“Ni muhimu kuepuka vinywaji kama pombe, ina tabia ya kutoa maji mengi na inachangia figo kufanya kazi haraka na kutoa maji mengi, tunashauri mtu asinywe pombe sana wakati wa joto.

Aidha, anasema wakati huu wa mvua kubwa watu wengine wanatumia nafasi ya mafuriko kutapisha vyoo hivyo umakini unahitajika katika mifumo ya mitaro kukaa sawa kama ni uchafu unaingia kwenye mfumo rasmi.

Dk Osati anasisitiza serikali inatakiwa kupuliza dawa za wadudu kuepusha malaria au homa ya dengu.

Kampeni kupanda miti nchi nzima

Aidha, Dk Osati anasema serikali iendelee kufanya kampeni ya kupanda miti kusaidia mazingira kwani mtu mmoja anategemea kupanda miti saba aishi na oksijeni vizuri.

“Kuna magonjwa yanatoka kwa wanyama kwenda kwa wanadamu kwa sababu ya mabadiliko hayo watu wanakula vitu ambavyo havitakiwi kuliwa. Muhimu kuhakikisha utunzaji wa mazingira na umakini wa afya kwa kila mtu,” anasisitiza.

Makala haya yamewezeshwa na Mesha na Ofisi ya Afrika ya IDRC Mashariki na Kusini.

Mwisho

Habari Zifananazo

Back to top button