WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax amewaagiza mabalozi wa Tanzania wanaowakilisha nje ya nchi wajipange na kufanya tathmini za mara kwa mara kuhusu mwelekeo wa sera za uhusiano wa kimataifa ili kulinda na kutetea maslahi ya taifa.
Amesema jumuiya ya kimataifa inakabiliwa na ushindani baina ya kimataifa katika matumizi ya rasilimali na maliasili chache zilizopo duniani, katika harakati za kujiletea maendeleo na ustawi, hivyo mabalozi hao hawana budi kujipanga na kufanya tathmini za mara kwa mara kubaini changamoto zilizopo na kuzifanyia kazi.
Ameyasema hayo katika hotuba yake iliyosomwa na Naibu Waziri Balozi Mbarouk Nassor Mabarouk, wakati akifungua mkutano wa mabalozi hao mjini Unguja jana.
Dk Tax alisema wizara yake imepewa dhamana ya kusimamia uhusiano na ushirikiano baina ya Tanzania na nchi nyingine, jumuiya za kikanda na kimataifa, hivyo alisema wanao wajibu wa kutoa ushauri kwa waliowapa dhamana hiyo kuhusu yale yote wanayoyaona nje ya mipaka ya Tanzania yawe mabaya au mazuri.
“Na katika hili nipende kusisitiza kuwa, kila wakati tujenge utamaduni wa kutathmini kwa kina mwenendo wa kidunia tukibainisha fursa na changamoto zilizopo ili ushauri tunaotoa uwawezeshe wadau wetu kufanya maamuzi sahihi,” alisema Dk Tax.
Aidha, aliwasisitiza mabalozi hao kufuatilia na kutoa taarifa katika hatua zote katika mnyororo wa maamuzi hadi kufanikisha uingiaji wa bidhaa husika katika soko hilo na kuhakikisha uendelevu wa jambo hilo.
Aliwapongeza mabalozi na wakurugenzi wa idara za kijiografia kwa kuwa wamekuwa wakifanya hivyo, na kutoa rai kwao kuendeleza hulka hiyo.
Alisema muundo wa utekelezaji wa majukumu yao unahusisha wadau wengi, hivyo hawana budi kuimarisha uratibu wa majukumu yao na kufuatilia utekelezaji wa makubaliano wa mikataba ya kimataifa pamoja na maelekezo ya viongozi wakuu katika taasisi za serikali na binafsi ili kupata mrejesho wa hatua iliyofikiwa.
“Tunatakiwa tuondokane na ile dhana ya kuwa sisi wabeba taarifa na badala yake tuwe ni wasimamizi wa masuala yote ambayo yamo ndani kwa dhamana yetu, kila wakati msisite kuuliza kwa ajili ya kupata taarifa na pia kukumbushia pale tunapohisi kuna hali ya kusuasua au kupungua kwa kasi ya utekelezaji,” alieleza.
Sambamba na hayo, aliwataka mabalozi hao kufanya kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano.
Alisisitiza juu ya umuhimu wa kuendeleza vikao vya mabalozi vya kikanda kubadilisha mawazo, huku akisema anafahamu kwamba wamekuwa wakifanya hivyo kila mara.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Balozi Joseph Sokoine alisema mkutano huu unaongozwa na kaulimbiu ya “Mwelekeo Mpya katika Kuimarisha Diplomasia ya Uchumi.”
Alisema kaulimbiu hiyo inaakisi na kuchagiza mwamko mpya wa utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje inayolenga kuinufaisha Tanzania kiuchumi na kijamii katika mazingira ya ushindani kimataifa.
Naye Naibu Katibu Mkuu, Fatma Rajabu alisema mkutano huo ni nyenzo muhimu katika kuimarisha utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi na Sera ya Mambo ya Nje.
Hivyo alisema mkutano huo utatoa fursa kwa mabalozi na menejimenti ya wizara kujadiliana, kubadilishana uzoefu miongoni mwao na kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Alisema mada mbalimbali zitajadiliwa zinazogusa maeneo mbalimbali yenye uhusiano wa moja kwa moja na majukumu ya wizara pamoja na kugusa utendaji wa kazi zao katika balozi zao.
Alizitaja mada hizo kuwa ni mwenendo wa dunia na taswira yake katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi, nafasi ya intelijensia katika kutekeleza diplomasia ya uchumi na fursa na mikakati ya kuiwezesha Tanzania kunufaika na Eneo Huru la Biashara Afrika.
Nyingine ni utaratibu wa mikopo ya uendeshaji wa vitega uchumi na ununuzi wa majengo na vitendea kazi balozini, mwelekeo mpya katika kuimarisha demokrasia ya uchumi tulipotoka, tulipo na tunapoelekea, fursa za kiuchumi Zanzibar katika maeneo ya uchumi wa buluu na uwekezaji katika miundombinu.
Pia kuimarisha uratibu wa shughuli za serikali yaani utekelezaji wa dira na mipango ya serikali kupitia mipango mikakati ya wizara na taasisi zilizo chini ya wizara na nafasi ya Chuo cha Diplomasia katika kuendeleza diplomasia ya Tanzania.
Naye Balozi wa Tanzania nchini Israel, Alex Kallua alisema amefurahishwa na mkutano huo ambao utawapatia nyenzo nzuri za kufanyia kazi pamoja na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuifungua nchi.
Alisema yapo mambo mengi ambayo yana tija kwa Jamhuri ya Muungano kwa upande wa Israel ambao wamepiga hatua kubwa katika maendeleo ya sayansi na teknolojia pamoja na mapinduzi ya kilimo na utalii.
Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Pareira Ame Silima alisema ni mkutano mzuri ambao utafungua fursa nyingi kwa Tanzania katika nchi wanazoziwakilisha, ambako matarajio kuyafikia malengo na mikakati ikiwamo masuala ya biashara na sayansi na teknolojia.
Mkutano huo unaohudhuriwa na mabalozi 49, unatarajiwa kuhutubiwa na Rais Samia Suluhu Hassan.