Maboresho Bandari ya Tanga yalipa

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa amesema maboresho makubwa yaliyofanywa na yanayoendelea kufanywa katika Bandari ya Tanga yameongeza ufanisi wa bandari hiyo na kuwa ndani ya miezi sita iliyopita wamekusanya mapato ya Sh bilioni 63.
Mbossa alisema hayo jana wakati akitoa maelezo mafupi kwa Rais Samia Suluhu Hassan aliyefanya ziara katika Bandari ya Tanga kujionea maboresho yaliyofanywa na serikali kupitia uwekezaji wa Sh bilioni 429 ulioimarisha uwezo na ufanisi wa bandari hiyo.
Alisema baada ya maboresho ya Bandari ya Tanga yaliyofikia Sh bilioni 428.8 yamezaa matunda na kwa kipindi cha miezi sita iliyopita, TPA imekusanya mapato zaidi ya Sh bilioni 63.
Alisema mapato hayo ni yale yanayohusu bandari pekee na kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao ndio wakusanyaji mapato wakuu nao wamekusanya kutoka chanzo hicho.
“Awali kabla ya maboresho haya makubwa Bandari yetu ya Tanga ilikuwa haisarifishi copper (shaba), sasa tunasafirisha na tumeshasafirisha tani 46,000,” alisema Mbossa.
Alisema hata uwezo wa bandari kuhudumia umeongezeka kutoka tani 400,000 hadi milioni 1.2 na kuwa mapato ya bandari yameongezeka kutoka Sh bilioni 21 hadi kufika Sh bilioni 71 kwa taarifa ya mwaka jana.
“TRA nao wameongeza mapato zaidi ya mara mbili kwa sababu meli kubwa zinaweza kuingia kutia nanga bandarini hapa na tumenunua mitambo ya kuhudumia meli kwa sasa zinakuja moja kwa moja,” alisema Mbossa.
Alisema mipango yao ya baadaye ni kuongeza gati la meta 300 na kuwa kupitia pia, ubia na sekta binafsi wataongeza gati la meta 600 kuongeza ufanisi zaidi katika bandari hiyo.
“Uwezo wetu wa bandari ni kuhudumia tani milioni tatu na tumedhamiria tuunganishe bandari na shughuli nyingine za kiuchumi kama sekta ya uzalishaji, kilimo na viwanda ,” alisema.
Alisema jumla ya gharama ya maboresho yote kwa bandari hiyo ni Sh bilioni 428.8 na kuwa awamu ya kwanza ilitolewa Sh bilioni 172 kwa lengo la kuongeza ujenzi wa njia ya maegesho ya meli na ununuzi wa mitambo.
Alisema awamu ya pili ya maboresho ilitolewa Sh bilioni 256.8 na kuwezesha bandari hiyo kuwa na muenekano huo mpya unaovutia watumiaji na kuongeza kiwango cha shehena kinachosafirishwa na kupokelewa.



