JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limebaini madereva 30 wakiwa na viwango vikubwa vya ulevi kati ya 179 waliopatikana na tabia na mienendo mibovu ya uendeshaji wa vyombo vya moto katika msimu wa sikukuu za Krismasi na mwaka mpya.
Madereva hao 30 wamefungiwa leseni zao za udereva kwa miezi sita ikiwa ni adhabu ya kukutwa na vilevi.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alieleza hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari kueleza mwenendo wa usalama katika kipindi cha sikukuu na matukio ya kihalifu yaliyochukuliwa hatua mwaka 2024.
Kamanda Muliro alisema sikukuu hizo zilikuwa za amani na utulivu kutokana na usimamizi wa sheria na kanuni zilizowekwa hususani sheria za usalama barabarani zilisimamiwa kikamilifu ili kudhibiti ajali na kwa kiasi kikubwa alisema walifanikiwa.
Alisema madereva hao 179 walituhumiwa na kufanyiwa vipimo kwa njia ya damu na hewa na kati yao, 30 waliokutwa na kiwango cha kikubwa cha ulevi cha zaidi ya miligramu 80, madereva 22 walitokea Kinondoni, sita Ilala na wawili Temeke.
Alisema kutokana na ukiukwaji huo wa sheria, wamewafungia leseni zao za udereva kwa kipindi cha miezi sita kwa mujibu wa sheria ya 28 Kifungu kidogo cha 3(b) cha Sheria ya Usalama Barabarani Sura ya 168 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Katika hatua nyingine, Kamanda Muliro alisema katika kipindi cha Novemba na Desemba mwaka jana, wamepata matokeo kutoka katika mahakama mbalimbali walizofikisha watuhumiwa wa makosa mbalimbali yakiwamo ubakaji na ulawiti na unyang’anyi wa kutumia silaha.
Muliro alisema miongoni mwa watuhumiwa hao ni Mkazi wa Mbagala, Sadick Foreni (30) na Mkazi wa Kibonde Maji, Joseph Ferdinandi waliohukumiwa kifungo cha maisha kwa kosa la ulawiti katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke.
Pia, washitakiwa wengine waliohukumiwa miaka 30 jela akiwamo mkazi wa Tabata, Ayubu Hatibu (32), mkazi wa Kitunda, Salmin Athuman (30), Henry Peter (36) na Ramadhani Amir (30).
Pia, alisema katika kuzuia matukio ya uhalifu kwa kufuatilia kwa ukaribu makundi yote ya watu wakiwamo wanaotumia dawa za kulevya na kufanya matukio ya uhalifu wamebaini watuhumiwa 250 waliokamatwa kuhusika, kusafirisha na kutumia dawa za kulevya.
Alisema Desemba 17, mwaka jana walimkamata mkazi wa Kipunguni Mashariki, Ally Ismail (22) kwa tuhuma za kuvunja na kukutwa na vitu mbalimbali vya wizi vikiwamo televisheni tatu, kompyuta za mezani tatu, kompyuta mpakato mbili, ving’amuzi vinne na ‘keyboard’ aina ya Dell nne.
Vilevile walimkuta na simu janja nane, simu ndogo sita, kamera aina ya Samsung moja, begi kubwa moja lenye nyaya, jiko moja, redio, mtungi wa gesi mmoja, mashine ya kunyunyizia dawa shambani moja na kuongeza kuwa atafakishwa mahakamani.