DESEMBA 9, 2024 Watanzania wanaadhimisha Miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika huku Tanzania ikifaidi matunda lukuki ya uhuru uliopatikana Desemba 9, 1961 kutoka katika makucha ya Waingereza.
Tangu mwaka huo, Tanzania imekuwa na kazi kubwa ya kulea uhuru maana uhuru ni kazi ndiyo maana, ili kujihakikishia uhuru endelevu, lazima kuhakikisha jamii inaunganisha nguvu na kupambana na kwa dhati kukabili maadui wakubwa watatu wa maendeleo yaani umaskini, ujinga na maradhi.
Kwa namna yoyote, ujinga huondolewa kwa njia ya elimu rasmi na isiyo katika mfumo rasmi tangu elimu ya awali, hadi elimu ya juu (Chuo Kikuu). Kuelekea maadhimihso hayo ya Jumatatu ijayo, makala haya yanajikita kutazama hatua zilizofikiwa katika elimu ya juu nchini tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika hadi sasa.
Uchunguzi wa HabariLEO umebaini kuwa, miongoni mwa mafanikio katika elimu ya juu nchini kwa kipindi cha Uhuru hadi sasa, ni pamoja na kuongezeka kwa fursa za masomo ya elimu ya juu na idadi ya wanafunzi wanaosoma katika vyuo vya elimu ya juu nchini.
Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Profesa Charles Kihampa, katika kipindi cha miaka 63 ya Uhuru wa Tanganyika, idadi ya vyuo vikuu nchini imeongezeka kutoka chuo kikuu kimoja mwaka 1961 hadi vyuo vikuu 50 mwaka 2024.
“Kihampa anasema katika kipindi cha uhuru wa Tanganyika, fursa mbalimbali za masomo zimeongezeka ikiwamo ongezeko la programu za masomo ambazo zimeruhusiwa kudahili wanafunzi wa shahada ya kwanza kutoka programu moja mwaka 1963/1964 hadi 860 mwaka 2024/2025,” anasema.
Anaongeza: “Wanaodahiliwa katika shahada ya kwanza wameongezeka kutoka 42 mwaka 1963/1964 hadi 137,781 mwaka 2024/2025 na idadi ya wanafunzi wanaosoma katika vyuo vya elimu ya juu imeongezeka kutoka 85 mwaka
1963/1964 hadi 314,643 mwaka 2022/2023. Haya ni mafanikio makubwa na serikali inastahili pongezi.”
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2005, TCU imekuwa ikitekeleza majukumu makubwa matatu ambayo ni kusimamia sheria, kanuni na taratibu za uanzishaji na uendeshaji wa vyuo vikuu nchini pamoja na kusaidia na kutoa miongozo kwa vyuo vikuu kuhusu uthibiti wa ubora wa vyuo vikuu, njia mbalimbali za uendeshaji wa vyuo, kuandaa na kuratibu mafunzo mbalimbali kwa wahadhiri, waendashaji na viongozi wa vyuo vikuu nchini.
Jukumu la tatu ni kutoa ushauri kwa umma, vyuo vikuu na serikali kupitia waziri mwenye dhamana ya elimu ya juu nchini kuhusu mabadiliko mbalimbali ya sayansi, teknolojia, sera na mwelekeo wa elimu ya chuo kikuu nchini na duniani kwa ujumla.
Umataifishaji elimu ya chuo kikuu nchini
Katika jitihada endelevu za kuboresha elimu ya chuo kikuu nchini na kuwezesha umataifishaji, Novemba 5, 2024 TCU imeidhinisha Mwongozo wa Taratibu za Udahili wa Waombaji Wenye Sifa za Kigeni katika Programu za Masomo katika Vyuo Vikuu Tanzania.
Profesa Kihampa anasema, “Mwongozo huu unabainisha ni namna gani vyuo vikuu nchini Tanzania vinaweza
kudahili wanafunzi wanaotaka kujiunga na vyuo hivyo kutoka nchi ambazo mifumo yao ya elimu haiendani na mfumo wa Tanzania.”
Anaongeza: “Hatua hii itachochea ongezeko la idadi ya wanafunzi wa kigeni wanaosoma katika vyuo vikuu nchini
Tanzania ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.” Kuimarishwa utoaji huduma za udahili, na utambuzi wa tuzo
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania imeimarisha mifumo yake ya kielektroniki inayotumika katika utoaji wa huduma
kwa wadau mbalimbali wa elimu.
Mifumo hiyo ni pamoja na mfumo wa pamoja wa kielekroniki kwa ajili ya kuratibu udahili wa shahada za kwanza
kwa vyuo vyote vya elimu ya juu nchini; Mfumo wa Utambuzi wa Tuzo za Wahitimu kutoka Vyuo Vikuu vya nje ya
Tanzania pamoja na Mfumo wa kuchakata maombi ya Hati ya Kutokuwa na Pingamizi kwa wananchi wanaotaka kwenda kusoma vyuo vikuu nje ya nchi.
“Uboreshaji huu umeongeza tija, ufanisi na kurahisisha utoaji huduma kwa kuwawezesha wananchi na wadau mbalimbali kupata huduma bora kwa haraka,” anasema.
Anatoa mfano akisema, “Muda wa uhakiki na utambuzi wa tuzo za nje ya nchi umepungua kutoka siku 14 za awali
hadi siku tatu. Aidha, waombaji wa udahili wanaweza kutuma maombi yao moja kwa moja kwenye vyuo husika na kuthibitisha vyuo wanavyopenda popote walipo bila kulazimika kusafiri kwenda chuoni.”
Aidha, kutokana na uboresho wa mifumo, taarifa mbalimbali zinazohusu elimu ya juu nchini sasa zinapatikana kwa
urahisi kwa ajili ya matumizi ya taasisi mbalimbali za umma na binafsi. Profesa Kihampa anasema,
“Kwa mfano, mfumo wa pamoja wa kielekroniki kwa ajili ya kuratibu udahili wa shahada za kwanza umeunganishwa na mfumo wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Zanzibar (ZHELB) na hivyo kurahisisha upatikanaji wa taarifa za udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu ambao ni wanufaika wa mkopo na kuharakisha utoaji wa mikopo ya wanafunzi husika.”
Uchunguzi umebaini kuwa, mifumo hii imewezesha upatikanaji wa taarifa na takwimu zinazohusu vyuo vikuu nchini
kama vile idadi ya wanafunzi, wahitimu, wahadhiri, viongozi, wafanyakazi waendeshaji na mitaala, hivyo kurahisisha
mipango ya serikali na wadau wa elimu ya juu nchini.
Wadau wengine wanaonufaika kutokana mifumo yao kuunganishwa na TCU kupata taarifa mbalimbali ni pamoja na Wizara ya Afya na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET).
Kuimarishwa programu za elimu kwa umma
Tume imeimarisha mifumo yake ya utoaji wa elimu kwa umma na kuwafikia wadau wengi zaidi. Elimu kwa umma imekuwa ikitolewa kupitia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutembelea wahitimu wa kidato cha sita waliopo kwenye mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) nchi nzima na kufanya mikutano nao kuwaelimisha kuhusu taratibu za udahili.
Aidha, wanafunzi wa Kidato cha Tano na Sita waliopo Unguja na Pemba wamekuwa wakinufaika na programu ya
elimu kwa umma ambapo tume imekuwa ikitembelea shule za sekondari zilizoko Zanzibar na kutoa elimu hiyo.
“Kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Tume imeendelea kushiriki Maonesho ya Wiki ya Elimu ya Juu Zanzibar yanayofanyika kila mwaka. Katika maonesho ya mwaka 2024, zaidi ya wananchi 16,783 wakiwemo wahitimu wa kidato cha sita walifikiwa na kupewa elimu ya chuo kikuu ndani na nje ya Tanzania,” anasema
Profesha Kihampa.
HabariLEO limekuwa likishuhudia Maonesho ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yakifanyika mfululizo kwa miaka 18 tangu mwaka 2005 hadi mwaka 2023. Profesa Kihampa anasema, “Maonesho haya yamekuwa na mwitiko
chanya kutoka taasisi nyingi ndani na nje ya nchi kwa kushiriki kuonesha huduma na bidhaa zao.”
“Aidha, idadi ya wananchi wanaotembelea maonesho haya imekuwa ikiongezeka hasa kutokana na vyuo vya elimu ya juu kutoa huduma ya udahili wakati wa maonesho hayo.”
Kama matunda ya uhuru wa Tanganyika (sasa Tanzania) Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania imeendelea kuimarisha mifumo yake ya uthibiti ubora na mifumo ya ndani ya vyuo
vikuu ili kuhakikisha vyuo vikuu vinaendana na mwelekeo wa nchi.
Kihampa anasema, “Tanzania imelenga kuwa taifa la watu wenye maarifa, ujuzi, weledi na uwezo wa kutatua
changamoto za kijamii na kiuchumi kwa manufaa ya wananchi wake ifikapo mwaka 2025 na kuifanya kuwa nchi ya uchumi wa kati unaochochewa na uwepo wa viwanda.”
Katika kuhakiki ubora, TCU imeimarisha mifumo yake ya ushauri na ukaguzi wa mara kwa mara, wa kawaida na wa
kushtukiza kuhakikisha elimu itolewayo na vyuo vikuu nchini, inakidhi viwango vya ubora kitaifa, kikanda, na kimataifa.
“Kwa mfano,” anasema, “Katika kipindi cha Julai 2021 hadi Februari, 2024 vyuo vikuu vyote 50 vilivyopo nchini vimekaguliwa na kupewa ushauri wa maeneo yanayohitaji kuboreshwa.”
Kuwajengea uwezo wahadhiri na viongozi wa vyuo vikuu
TCU imeendelea kuandaa na kuratibu mafunzo kwa viongozi, wahadhiri na maofisa wa vyuo vikuu vya umma na binafsi nchini kuwajengea uwezo katika usimamizi na uendeshaji wa taasisi zao.
“Kwa miaka 19 ya utendaji kazi wa TCU viongozi na wanataaluma 1,742 wamenufaika na mafunzo hayo aliyolipiwa na Serikali kwa asilimia 100,” anasema.