Mahakama yazuia live ushahidi kesi ya Lissu

DAR ES SALAAM; MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeamuru maelezo ya mashahidi na idadi ya vielelezo katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia (CHADEMA), Tundu Lissu kutopelekwa mubashara, kuchapisha wala kuhaririwa isipokuwa kwa amri ya mahakama.
Mahakama hiyo imeeleza amri huyo imezingatia uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu Agosti 4,mwaka huu na Jaji Hussein Matembwa ulioamuru kuhifadhi utambulisho wa mashahidi wa kiraia kulindwa, ikisisitiza kupeleka maudhui mubashara kuchapisha na kueneza katika mitandao ya kijamii kunaweza kufumbua utambulisho wao.
Amri hiyo imetolewa leo Agosti 18,2025 na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga shauri hilo lilipopelekwa kwa ajili kutolewa amri hizo pamoja na kusomwa maelezo ya mashahidi na vielelezo vitakavyotumika katika shauri hilo litakapopelekwa Mahakama Kuu.
Awali, Wakili wa serikali Nassoro Katuga alidai shauri kilipelekwa kwa ajili ya kusomwa maelezo ya mashahidi ili shauri lipelekwe mahakama kuu kwa mujibu wa kifungu cha 263 cha sheria Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), hivyo walikuwa tayari kuendelea na mshitakiwa alikuwa tayari pia.
Hakimu Kiswaga amesema katika kikao cha mahakama kilichopita walifanya mawasilisho ya maombi yanayohusiana na mwenendo wa Kupeleka shauri hilo Mahakama Kuu kwamba upande wa Jamhuri uliwasilisha maombi ya kuomba mahakama isirushe moja kwa moja au kuchapisha kwa umma mwenendo wa maelezo ya mashahidi na upande wa utetezi ulipinga vikali.
“Agosti 4,mwaka huu mahakama kuu ilitoa maagizo ya kulinda mashahidi ambao ni raia wa kawaida kuhusiana na shauri 8607/2025 linalomkabili Lissu maagizo hayo yalikuwa yanajumuisha kutokufichua utambulisho wa mashahidi na taarifa zitakazopelekea kuwafichua,” amesema Hakimu.
Ameongeza uamuzi huo ulijumuisha majina ya utani, pia kuhariri taarifa ambazo zitaweza kufichua utambulisho wa mashahidi, pia jamhuri iliitaarifu mahakama kuwa imeshasajili Mahakama Kuu shauri hilo na kuomba taarifa hizo zisichapishwe ili kulinda utambulisho wa mashahidi.
Amesema masharti, matendo na mamlaka ya kusimamia Mahakama Kuu yanapaswa kufuatwa pale maagizo yanapotolewa, akisisitiza kuwa mahakama kwa kawaida ni za wazi kwa umma, lakini mahakama inapaswa kulinda haki za mashahidi, usalama pamoja na familia zao.
Hakimu Kiswaga amesema kwa msingi huo maelezo hayo ya mashahidi hayatopelekwa mbashara wala kuchapishwa katika mitandao yoyote ya kujamii wala kuhaririwa na kutofanya hivyo hakutomzuia mshitakiwa kusikiliza bali kunazuia ueneaji wa moja kwa moja unaoweza kupeleka kufichuliwa kwa mashahidi.
Amesisitiza ili taarifa hizo kurushwa au kuchapishwa kunapaswa maombi yapelekwe mahakamani na mahakama itoe kibali, pia maombi yoyote ya kuchapishwa inapaswa yaombwe na uamuzi utolewe alisema maelezo hayo yataendelea katika mahakama ya wazi mshitakiwa atasikiliza kama ilivyoelezwa.
“Uchezaji wa moja kwa moja, utangazaji au usambazaji wa moja kwa moja au aina nyingine ya uenezaji mahakama inazuia hadi pale itakapotoa amri nyingineyo itakayotolewa na mahakama hii au mahakama kuu,” amesema Hakimu,
Ameongeza; “Pia kuchapisha kunakili au kusambaza nyaraka zozote za ushahidi zinazoonesha eneo, mahali au utambulisho wowote wa shahidi unakatazwa na ni marufuku bila idhini ya mahakama hii, kila kituo cha habari au wanahabari wanaotaka kuchapisha taarifa ya kwenda mahakama kuu kitaleta kibali”.
Pia amesema Mahakama inautaka upande wa Jamhuri kuhakikisha kabla taarifa yeyote haijasomwa iwe imezingatia taarifa za mahakama kuu kwa kuchakata na kuhariri taarifa zote zinazoweka kufichua utambulisho wa mashahidi.
Pia amesisitiza kila mtu au chombo cha habari kitakachokwenda kinyume na uamuzi huu hatua stahiki zitachukuliwa kwa kuwa ilikuwa ni amri ya Mahakama Kuu, akisema kanuni ya mahakama kuendeshwa wazi inabaki kuwa muhimu kwa mfumo wa haki lakini inapsawa kutolewa iwapo kuna hatari iliyoonyeshwa dhidi ya mashahidi.