Majaji wajengewa uwezo kukabiliana na uhalifu

DAR ES SALAAM: Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Italia ( Sant’Anna School of Advanced Studies -Scuola) kupitia ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Italia, kimeanza kutoa mafunzo ya siku tatu kwa majaji, mahakimu wa ngazi mbalimbali na waendesha mashtaka wa Tanzania kuhusu ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na makosa ya jinai yanayovuka mipaka.

Mafunzo hayo yamefunguliwa leo Sept 29, 2025 na Balozi wa Italia nchini Tanzania Giuseppe Sean Coppola na yanafanyika Mahakama Kuu – Kituo Jumuishi cha Masuala ya familia Temeke mkoani Dar es Salaam. Wawezeshaji wa Mafunzo hayo ni Majaji kutoka Tanzania pamoja na wahadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Italia.

Lengo la mafunzo hayo ni kuimarisha uelewa na uwezo wa maofisa hao katika kushughulikia makosa hayo ya jinai hususani maeneo ya ushirikiano wa Kimahakama juu ya urejeshaji wa watuhimiwa na kusaidiana kisheria kati ya nchi mbalimbali kwenye makosa ya jinai.

Katika neno lake la utangulizi, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania – Kituo hicho Jumuishi, Mwanabaraka Mnyukwa amebainisha kuwa umuhimu wa mafunzo haya ni kuimarisha mifumo ya ushirikiano wa Kimataifa katika kushughulikia upelelezi na uendeshaji wa mashauri ya kimataifa yanayovuka mipaka.

“Mafunzo haya yatawapatia washiriki kuhusu namna nchi na vyombo vyao, zinaweza kushirikiana katika kushughulikia uhalifu wa kuvuka mipaka unaoharibu amani ya dunia, usalama, uchumi na maendeleo ya jamii,” amesema.

Na katika hotuba yake ya ufunguzi, Balozi Coppola amesema kuwa kupitia mafunzo hayo washiriki wa Tanzania na wa Italia watatoka na uelewa wa pamoja katika kushughulia uhalifu huo, akibainisha kuwa nchi yake ni miongoni wa waathirika wakubwa wa uhalifu huo.

“Mtandao wa uhalifu unaouvuka mipaka ni tatizo kubwa duniani, na umekuwa na athari kubwa kwa jamii, hivyo tunahitaji kuimarisha ushirikiano kati ya majaji, mahakimu na waendesha mashtaka wa Tanzania na Italia, ili tuwe na uelewa mmoja wa jinsi ya kukabiliana na mtandao huo,” amesema Balozi Coppola.

Ufunguzi huo umehudhuriwa pia na Mkurugenzi wa mradi wa Utawala wa Sheria na Ushirikiano wa Mahakama ambaye pia ni Profesa Msaizidi wa Scuola Lorenzo Gasbarri pamoja na viongozi wengine.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button