WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza halmashauri nchini zitumie fedha za makusanyo ya ndani kutekeleza miradi ya maendeleo badala ya kusubiri fedha kutoka serikali kuu.
Majaliwa alitoa agizo hilo jana alipokagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa sita katika Shule ya Sekondari ya Mwandege wilayani Mkuranga, Pwani.
Taarifa ya ofisi ya Waziri Mkuu ilieleza kuwa Majaliwa alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Mwantumu Mgonja kutenga Sh milioni 120 kutoka kwenye mapato ya ndani kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo la utawala katika shule hiyo ifikapo Januari, mwakani.
Majaliwa alisema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kuhudumia Watanzania ili kusaidia kuchochea shughuli za maendeleo katika maeneo yao.
“Huu ni wakati wa kufanya kazi, nimeridhika na viwango vya ujenzi wa vyumba madarasa katika shule hii, endeleeni kusimamia viwango kwenye miradi mingine, twende na matakwa ya Rais wetu na kumsadia kutimiza maono yake ya kuwahudumia Watanzania”alisema.
Majaliwa alisema mipango ya Rais Samia ni kuhakikisha serikali inawafikia Watanzania popote walipo hadi vitongojini kwa kupeleka huduma za kijamii zikiwamo za afya, maji, shule, umeme na mawasiliano.
Aidha, aliwataka wakulima nchini kutumia mvua za mwanzo kuanza kujishughulisha na kilimo.
“Mvua za kwanza ndio za kupandia, twende tukaanze kazi ya kilimo, tupande mazao yenye uwezo wa kuota kwa muda mfupi ili yaweze kuiva na kutusaidia kupata chakula,” alisema Majaliwa.
Pia aliagiza watendaji wa serikali kuzungumza na wakulima kuhusu kutumia vizuri chakula kilichopo kiweze kuwasaidia kufika msimu ujao wa mavuno. Naibu Waziri Ofisi ya Rais (Tamisemi) Dk Festo Dugange alisema Mkoa wa Pwani ulipewa Sh bilioni 6.8 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 341.
“Wananchi wa Mkuranga niwahikishie kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria na anafanya kwa vitendo kutuondolea adha ya vyumba vya madarasa,”alisema Dugange.
Mbunge wa Mkuranga na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdala Ulega alimshukuru Rais Samia kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Mkuranga na mkoa kwa ujumla.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa, Ofisa Elimu Idara ya Sekondari, Benjamin Majoya, alisema Mkuranga imepokea fedha za ujenzi wa vyumba vya madarasa 132 ya kidato cha kwanza kwa mwaka 2023 katika shule 26 za sekondari yenye thamani ya Sh bilioni 2.64.
Majoya alisema kukamilika kwa vyumba hivyo vya madarasa na vilivyopo, kutawezesha wanafunzi 10,800 kupata nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2023 wilayani Mkuranga.
Majaliwa jana alianza ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuzungumza na watumishi mkoani Pwani.